Nani ana haki zaidi ya kutendewa wema kati ya baba na mama?

Swali: Inajuzu kumfadhilisha mzazi mmoja juu ya mwingine ilihali wote wawili bado wako hai kama kwa mfano akamjengea msikiti mmoja wao?

Jibu: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alijibu wakati alipoulizwa swali lisemalo:

“Ni nani mwenye haki zaidi ya kutendewa wema?” Akajibu: “Mama yako.” Akauliza: “Kisha nani?” Akajibu: “Mama yako.” Akauliza tena: “Kisha nani?” Akajibu: “Mama yako.” Akauliza tena: “Kisha nani?” Akajibu: “Baba yako.”

Ni sawa akafadhilishwa mama inapokuja katika kutendewa wema kabla ya baba. Lakini mtoto akijua kwamba iwapo baba yake atamuona anamfadhilisha mama yake kabla ya baba yake ataingiwa na kitu moyoni, basi katika hali hii anatakiwa asimdhihirishie baba yake kwamba amemfadhilisha mama yake kwa kitu chochote. Haya ni kwa sababu ya kuzuia madhara. Kwa sababu ya baadhi ya kina baba hawawezi kustahamili kuona mtoto anamfadhilisha mama yake juu yake na wanachukulia hilo kama ni utovu wa adabu. Mambo yakiwa hivo basi epuka kufanya hivo na wala usimweleze kuwa wewe umemfadhilisha mama yako juu yake kwa kitu chochote. Kwa kufanya hivo madhara yataondoka kwa idhini ya Allaah.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (44) http://binothaimeen.net/content/1019
  • Imechapishwa: 20/02/2019