Namna ya kufanya Tayammum


Swali: Tunaomba utubainishie njia sahihi ya kufanya Tayammum?

Jibu: Tayammum sahihi ni kama alivosema Allaah:

وَإِن كُنتُم مَّرْضَىٰ أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ أَوْ جَاءَ أَحَدٌ مِّنكُم مِّنَ الْغَائِطِ أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ فَلَمْ تَجِدُوا مَاءً فَتَيَمَّمُوا صَعِيدًا طَيِّبًا فَامْسَحُوا بِوُجُوهِكُمْ وَأَيْدِيكُم مِّنْهُ

”Mkiwa wagonjwa au mko safarini au mmoja wenu akitoka chooni au mmewagusa wanawake, kisha hamkupata maji, basi fanyeni Tayammum kwa ardhi ilio safi panguseni kwayo nyuso zenu na mikono yenu.”[1]

Kilichosuniwa ni pigo moja usoni na mikononi. Namna yake ni kwamba apige udongo kwa mikono yake pigo moja kisha afute kwayo uso na viganjan vya mikono. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kumwambia ´Ammaar bin Yaasir (Radhiya Allaahu ´anh):

”Hakika si vinginevyo ilikuwa inakutosha kufanya kwa mikono yako namna hii.”

Kisha akapiga ardhi kwa mikono yake na akafuta kwayo uso na viganja vya mikono yake.

Ni sharti udongo uwe msafi. Haikusuniwa kufuta sehemu ya juu ya mikono. Bali inatosha kufuta uso na viganja vya mikono kutokana na Hadiyth iliyotajwa.

Tayammum inachukua sehemu ya maji katika kuondosha hadathi kwa mujibu wa maoni sahihi. Akishafanya Tayammum basi ataswali kwa Tayammum hii swalah zilizopendekezwa, zilizofaradhishwa, za hivi sasa na za huko mbele muda kuwa bado yuko na twahara mpaka pale atapopata hadathi, apate maji akiwa ni mwenye kuyakosa au mpaka pale atakapoweza kuyatumia akiwa alishindwa kuyatumia. Kwa hivyo Tayammum ni yenye kutwaharisha inayoshika nafasi ya maji, kama ambavo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliita kuwa ni yenye kutwahirisha.

[1] 05:06

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (05/66)
  • Imechapishwa: 16/02/2021