Nafasi kubwa ya zakaah katika Uislamu


Swali: Ni ipi hukumu ya zakaah katika Uislamu? Ni lini ilifaradhishwa?

Jibu: Zakaah ni moja ya faradhi za Uislamu ambazo Uislamu umejengeka juu yake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Uislamu umejengeka juu ya vitano; kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kuhiji Nyumba tukufu ya Allaah.”[1]

Zakaah ni wajibu kwa maafikiano ya waislamu. Yule mwenye kupinga ulazima wake basi amekufuru muda wa kuwa sio punde ameingia katika Uislamu au amekulia huko jangwani ambako hakuna elimu na wanazuoni. Katika hali hiyo atapewa udhuru, lakini hata hivyo anatakiwa kufunzwa. Akiendelea kupinga baada ya kufunzwa basi amekufuru na ameritadi.

Kuhusu yule ambaye amekataa kutoa zakaah kwa sababu ya ubakhili na kuchukulia wepesi, wanazuoni wametofautiana. Wako waliosema kuwa anakufuru, na ni moja ya upokezi kutoka kwa Ahmad. Wengine wakasema kuwa hakufuru. Haya ndio maoni sahihi. Hata hivyo amefanya dhambi kubwa. Dalili kuonyesha kuwa hakufuru ni maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakuna mtu aliye na dhahabu au fedha na asiitolei zakaah isipokuwa siku ya Qiyaamah atapewa sahani za Moto zilizochochewa kwenye Moto wa Jahannam kisha apigwe nazo kwenye mbavu zake, paji lake la uso na kwenye mgongo wake. Kila zinapopoa zinatiwa moto tena kwa siku moja ambayo ni sawa na miaka 50.000 mpaka pale waja watakapohukumiwa. Kisha aone njia yake; ima kuelekea Peponi au kuelekea Motoni.”[2]

Ikiwa kuna uwezekano akaona njia yake ya kuelekea Peponi basi hiyo ina maana kwamba sio kafiri, kwa sababu hakuna uwezekano wa kuingia Peponi kwa ambaye ni kafiri. Hata hivo mtu huyu ametenda dhambi kubwa kwa kule kutotoa kwake zakaah kutokana na ubakhili na kuchukuli wepesi. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَا يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَّهُم ۖ بَلْ هُوَ شَرٌّ لَّهُمْ ۖ سَيُطَوَّقُونَ مَا بَخِلُوا بِهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ وَلِلَّـهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۗ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ

“Wala wasidhani kabisa wale wanaofanya choyo kwa yale aliyowapa Allaah katika fadhilah Zake kwamba hayo ni kheri kwao, bali ni shari kwao. Watafungwa kongwa yale waliyoyafanyia choyo siku ya Qiyaamah. Na ni Wake Allaah pekee urithi wa mbingu na ardhi. Na Allaah kwa yale myafanyayo ni Mwenye khabari za ndani kabisa.”[3]

وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلَا يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ يَوْمَ يُحْمَىٰ عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَىٰ بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنُوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ ۖ هَـٰذَا مَا كَنَزْتُمْ لِأَنفُسِكُمْ فَذُوقُوا مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ

“Na wale wanaolimbikiza dhahabu na fedha na wala hawazitoi katika njia ya Allaah, basi wape bishara ya adhabu iumizayo. Siku zitakapopashwa katika Jahannam na kwazo vikachomwa moto vipaji vyao na mbavu zao na migongo yao [huku wakiambiwa]: “Haya ndio mliyoyalimbikiza kwa ajili ya nafsi zenu. Hivyo basi, onjeni yale mliyokuwa mkiyalimbikiza.”[4]

Kwa hivyo ni lazima kwa muislamu kumshukuru Allaah juu ya neema ya mali na aitolee zakaah yake ili Allaah amzidishie mali yake na aitie baraka.

Ama mahapa ilipofaradhishwa zakaah ni Makkah, kama yalivyo maoni yenye nguvu zaidi, lakini vigezo na hukumu zake zilizowekwa Madiynah.

[1] al-Bukhaariy (8) na Muslim (16).

[2] Muslim (987).

[3] 3:180

[4] 9:34-35

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (18/13-15)
  • Imechapishwa: 04/08/2021