Mzee wa miaka 65 amemtaliki mkewe mara sitini

Swali: Baba yangu amefikisha miaka sitini na tano. Miaka mbili ya mwisho amebadilika kiasi kikubwa. Amemtaliki mama yangu kwa kumwambia “Nimekutaliki mara sitini”. Mara anamtaliki na mara anamrejea. Ni yepi maoni yako? Je, mama arudi kwake kwa vile amefikisha miaka yote hii na yeye ni mwenye kuhitajia mtu wa kumwangalia?

Jibu: Ikiwa maneno haya yanayomtoka haelewi anachokisema, basi talaka haipiti. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Talaka haipiti katika hali ya kutokwa na akili.”

Hili ni dalili ya wazi kuhusu talaka. Vilevile Allaah (Ta´ala) amesema:

لَا يُؤَاخِذُكُمُ اللَّـهُ بِاللَّغْوِ فِي أَيْمَانِكُمْ

“Allaah hatokuchukulieni kwa viapo vyenu vya upuuzi.”[1]

Mtu huyu akiwa hajui kile anachokisema lakini dhiki ikampelekea akataliki, basi kimsingi ni kwamba hana talaka kabisa. Si moja wala talaka sitini. Ama akiwa anaelewa na akamwambia kwamba amemtaliki mara sitini, basi tunamwambia kwamba inamtosha kutaliki mara tatu na hizo khamsini na saba ni zake. Kwa hivyo wewe peleleza.

Uhalisia wa mambo ni kwamba umri wa miaka sitini na tano haupelekei mtu akapatwa na ugonjwa wa uzee na kutokwa na akili. Isipokuwa ikiwa kama mtu amepatwa na maradhi kichwani mwake. Hapo inawezekana. Lakini kikawaida umri huu haupelekei katika ugonjwa wa uzee na kutokwa na akili.

Kwa ufupi ni kwamba ikiwa baba wakati aliposema maneno haya alikuwa anamaanisha na anaelewa anachokisema, basi talaka imepita. Zimepita talaka tatu au moja tu? Katika hili kuna tofauti. Ama akiwa si mwenye kuelewa anachokisema, basi talaka haikupita.

[1] 05:89

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (61) http://binothaimeen.net/content/1390
  • Imechapishwa: 09/06/2020