Mzazi anamzuia mvulana kwenda msikitini


Swali: Mimi ni kijana niliye na miaka kumi na sita. Baba yangu ananizuia kuswali msikitini na kuswali swalah ya ijumaa. Angeliweza basi angelikataza kuswali kabisa. Anajua Shari´ah inavosema juu ya jambo hili. Sambamba na hilo anajaribu kunivuta kutoka katika hali niliyomo na kunipeleka katika hali ya maasi na maovu. Je, nimtii?

Jibu: Hapana shaka kwamba kumtii mzazi ni jambo la lazima. Allaah ndiye ambaye kawajibisha kumtii mzazi. Lakini hata hivyo si lazima kumtii mzazi katika kila jambo. Ni wajibu kumtii tu katika yale mambo ambayo ndani yake hakuna kumuasi Allaah na Mtume Wake. Ama ikiwa katika kumtii ndani yake kuna kumuasi Allaah na Mtume Wake, itakuwa haijuzu kwa mtoto kumtii baba yake katika jambo hilo. Kujengea juu ya hili haijuzu kwako kuacha swalah ya mkusanyiko wala swalah ya ijumaa kwa sababu baba yako kukuzuia. Ni lazima kwako kupupia juu ya swalah ya mkusanyiko na swalah ya ijumaa kwa kila njia utayoweza.

Jengine ni kwamba baba yako yuko na haki juu yako: unatakiwa kumnasihi, kumwelekeza na kumpa zawadi ya vitabu vyenye manufaa ambavyo anaweza kusoma. Pengine Allaah akamwongoza na akamrudisha katika msimamo na kuwa imara juu ya haki. Huu ni wema mkubwa wa kumfanyia mzazi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb (13) http://binothaimeen.net/content/6781
  • Imechapishwa: 02/02/2021