Mwenye hedhi na nifasi kuchelewesha kulipa mpaka wakafikiwa na Ramadhaan nyingine


Swali: Ni ipi hukumu ya mwanamke mwenye hedhi na nifasi wakichelewesha kulipa mpaka kukaingia Ramadhaan nyingine? Ni kipi kinachowalazimu?

Jibu: Ni wajibu kwa mwenye hedhi na nifasi kuacha kufunga wakati watapopata damu. Haijuzu kwao kufunga wala kuswali wakati wa hedhi na nifasi. Wala hayasihi kwao. Ni wajibu kwao kulipa swawm na si wajibu kwao kulipa swalah. Imethibiti kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhumaa) kwamba ameulizwa:

“Je, mwenye hedhi analipa swawm na swalah?” Akasema: “Tulikuwa tukiamrishwa kulipa swawm na hatuamrishwi kulipa swalah.”[1]

Kumeafikiana juu yake.

Wanachuoni (Rahimahumu Allaah) wameafikiana juu ya yale yaliyotajwa na ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) juu ya uwajibu wa kulipa swawm na kutolipa swalah kwa haki ya mwenye hedhi na mwenye nifasi. Hiyo ni rehema kutoka kwa Allaah na kuwasahilishia. Kwa sababu swalah ni yenye kujirudi kwa siku mara tano na katika kuilipa kuna uzito.  Lakini swawm kwa mwaka ni mara moja – nayo ni funga ya Ramadhaan – na katika kuilipa hakuna uzito juu yake.

Mwenye kuchelewesha kulipa mpaka kukaingia Ramadhaan nyingine pasi na udhuru wa Kishari´ah, basi ni lazima kwake kutubu kwa Allaah kutokana na hilo na alipe pamoja vilevile na kulisha maskini mmoja kwa kila siku moja. Kadhalika mgonjwa na msafiri wakichelewesha mpaka kukaingia Ramadhaan nyingine pasi na udhuru wa Kishari´ah, basi ni lazima kwao kulipa na kutubu pamoja vilevile na kulisha masikini mmoja kwa kila siku moja. Ama ikiwa maradhi au safari itaendelea mpaka Ramadhaan nyingine basi ni wajibu kwao kulipa tu pasi na kulisha baada ya kupona kutokamana na maradhi au watapofika kutoka safarini.

[1] Muslim (508).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (15/181-182)
  • Imechapishwa: 18/05/2018