Mwanamke na daktari wa kiume


Swali: Unasemaje juu ya suala ambalo mara nyingi huuliziwa na ambalo limekuwa ni kama kero kwa waislamu. Nalo si jengine inahusiana na suala la mwanamke na daktari wa kiume. Ni yepi unawanasihi dada wa Kiislamu juu ya hilo na vivyo hivyo wasimamizi wao?

Jibu: Hapana shaka kwamba suala la mwanamke na daktari wa kiume ni suala muhimu. Ukweli wa mambo ni kwamba linachosha sana. Lakini Allaah akimruzuku mwanamke kumcha Allaah na elimu basi anaichunga nafsi yake na atatilia umuhimu jambo hilo. Haifai kwake kukaa chemba na daktari wa kiume kama ambavo haifai kwa daktari wa kiume kukaa naye chemba. Kumetoka amri na maagizo kutoka kwa watawala yanayowazuia kufanya hivo. Kwa hiyo ni lazima kwa mwanamke kutilia umuhimu jambo hili na pia ajitahidi kutafuta madaktari wa kike wanaotosheleza. Akiwapata ni sawa na hivyo kutakuwa hakuna haja ya daktari wa kiume.

Lakini haja ikipelekea kutibiwa na daktari wa kiume kwa sababu ya kukosekana madaktari wa kike, basi wakati wa haja kutakuwa hakuna makatazo ya kujifunua na kutibiwa. Hili ni miongoni mwa mambo yanayofaa wakati wa haja. Lakini kujifunua kusifanyike mahali pa chemba. Bali matibabu yafanyike mbele ya Mahram au mume wake ikiwa ujifunuaji unahusiana na mambo ya juujuu kama mfano wa kichwa, mkono, mguu na mfano wa hayo. Na ikiwa viungo vinavyofunuliwa ni vile vya nyuchi, basi awe pamoja na mume wake ikiwa yuko na mume au awe pamoja na mwanamke mwingine. Kufanya hivo ndio bora na salama zaidi. Au vilevile anaweza kuhudhuria muuguzi wa kike au wauguzi wawili wa kike. Lakini akipatikana mwanamke mwingine ambaye atakuwa pamoja naye – mbali na muuguzi wa kike – ndio itakuwa bora, salama zaidi na kuepuka mbali na mashaka. Ama kukaa faragha ni jambo halijuzu.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (05/392)
  • Imechapishwa: 23/01/2021