Mwanamke mwenye hedhi kuingia msikitini kutoa darsa kwa wanawake wenzio

Swali: Je, inajuzu kwa mwanamke mwenye hedhi kuingia Msikitini kutoa mihadhara kwa wanawake wenzake?

Jibu: Kumepokelewa Hadiyth kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mimi sikuhalalisha Msikiti kwa mwenye hedhi wala janaba.”

Lakini Hadiyth hii ni dhaifu. Na imethibiti katika Swahiyh ya kwamba kuna mwanamke ambaye alikuwa anafanya kazi Msikitini na analala Msikitini. Na mwanamke huyu ada yake na tabia yake ilikuwa ni kama wanawake wengine (wanaopata hedhi). Alikuwa anafanya kazi Msikitini na akiishi humo. Pamoja na hivyo hakuwahi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumtoa wala kumkataza kutoingia humo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anamwambia vile vile ´Aaisha (Radhiya Allaahu ´anha) hali ya kuwa alikuwa ni mwenye hedhi alipokuwa katika Hajj:

“Fanya kama anayofanya mwenye kuhiji, lakini usitufu Ka´abah.”

Anasema tena Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia ´Aaishah pindi alipomwambia amsaidie kumpokeza kitu, akasema ´Aaishah:”Mimi ni mwenye hedhi.” Akasema (´alayhis-Salaam):

“Hedhi yako haiko mikononi mwako.”

Lililo la dhahiri ni kuwa, hakuna ubaya mwanamke mwenye hedhi kuingia Msikitini kwa sharti asiuchafue Msikiti. Pengine akatokwa na kitu, ni lazima ajisitiri na kitu vizuri ili asiuchafue Msikiti na awafanyie Darsa dada zake.

  • Mhusika: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://olamayemen.net/Default_ar.aspx?ID=3134
  • Imechapishwa: 20/02/2018