Swali: Inajuzu kwa mwanamke kudhihirisha kitu katika mwili wake kama kisigino chake, kifua chake na mfano wa hayo mbele ya Mahaarim zake kama watoto wake wa kiume, kaka zake na mfano wa hao? Je, kuna tofauti baina ya hayo kati ya Mahaarim wa kiume na wa kike?

Jibu: Hakika mimi nasikitika sana kutafiti mambo kama haya. Wake wa wanaume hapo kale walikuwa ni wenye kujisitiri, kuvaa Hijaab na walikuwa na haya. Lakini pindi watu walipokithiri kuchanganyika na wengine wenye kutoka miji ya nje au pamoja na wale ambao mtu amesafiri kwenda katika miji yao, ndipo kukawa matatizo na tafiti kama hizi. Haina shaka kuwa kila ambavyo mwanamke atakuwa ni mwenye kujisitiri kwa mambo kama haya ambayo yanaweza kuamsha hisia – hata kama itakuwa mbele ya Mahaarim zake – ndio bora zaidi. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) katika kijitabu chake “Libaas-ul-Mar-ah” amesema ya kwamba wanawake wa Maswahabah majumbani mwao walikuwa wakivaa mavazi yenye kusitiri kuanzia mikono yao mpaka kwenye miguu yao. Kwa hiyo anakuwa si mwenye kuonesha si miguu, mikono wala chengine.

Lakini lau tutakadiria ya kwamba mwanamke amefunua mikono yake au visigino vyake kwa sababu ya kazi za nyumbani na mbele yake wapo Mahaarim zake au wanawake wengine hakuna neno. Ama kuvaa nguo fupi inayoishia kwenye magoti au chini kidogo ya hapo, kunachelea juu yake akawa ni mwenye kuingia ndani ya maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kuna aina mbili ya watu wa Motoni sijawaona kamwe; watu wenye bakora kama mkia wa ng´ombe wanapiga nayo watu na wanawake ambao wamevaa na wako uchi, Muumiylaat Maailaat. Vichwa vyao ni kama nundu ya ngamia. Hawatoingia Peponi na wala hawatoinusa harufu yake. Harufu yake inapatikana umbali wa kadhaa na kadhaa.”

Nasaha zetu kwa dada zetu wanawake wajiepushe na mavazi haya. Wavae mavazi ya kusitri. Nasaha zetu vilevile kwa wasimamizi wao wasiwaache wanawake wakavaa mavazi yanayoenda kinyume na Shari´ah.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (11)
  • Imechapishwa: 03/05/2020