Swali: Kuna tofauti kati ya swalah ya mwanamke na mwanaume kwenye Sujuud katika swalah?

Jibu: Hakuna tofauti kati ya mwanamke na mwanaume katika Sujuud, hakuna tofauti kati ya mwanamke na mwanaume katika Rukuu´ na hakuna tofauti kati ya mwanamke na mwanaume katika kukaa. Mwanaume ni kama mwanamke; isipokuwa tu wao hawatakiwi kunyanyua sauti. Kwa msemo mwingine ni kwamba si katika sunnah mwanamke kusoma kwa sauti hata kama itakuwa ni swalah ya usiku. Vivyo hivyo imamu anapokosea wao hawatakiwi kusema “Subhaan Allaah” na badala yake wanatakiwa kupiga makofi. Kusema “Subhaan Allaah” ni kwa wanaume na kupiga makofi ni kwa wanawake.

Kimsingi ni kuwa wanaume na wanawake ni sawa katika hukumu za Allaah (Ta´ala) isipokuwa kukiwepo dalili inayoteganisha. Hiki ni kidhibiti au kanuni ambayo muislamu anaweza kufaidika nayo. Kimsingi ni kuwa wanaume na wanawake ni sawa katika hukumu na Shari´ah ya Allaah (Ta´ala) isipokuwa kukiwepo dalili ya wazi inayofahamisha kutofautisha kati ya mwanaume na mwanamke. Kwa ajili hiyo mwenye kumtuhumu machafu mwanaume ambaye ametakasika anatakiwa kupigwa bakora thamanini? Ndio, anatakiwa kupigwa bakora thamanini. Pamoja na kuwa Aayah iliyokuja inawahusu wanawake:

وَالَّذِينَ يَرْمُونَ الْمُحْصَنَاتِ ثُمَّ لَمْ يَأْتُوا بِأَرْبَعَةِ شُهَدَاءَ فَاجْلِدُوهُمْ ثَمَانِينَ جَلْدَةً وَلَا تَقْبَلُوا لَهُمْ شَهَادَةً أَبَدًا ۚ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ إِلَّا الَّذِينَ تَابُوا مِن بَعْدِ ذَٰلِكَ وَأَصْلَحُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

“Wale wanaowatuhumu wanawake wenye kujichunga na machafu kisha hawaleti mashahidi wanne, basi wapigeni bakora themanini na wala msikubali ushahidi wao kamwe – na hao ndio mafasiki! Isipokuwa wale waliotubu baada ya hayo na wakatengemaa, basi hakika Allaah ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.”[1]

Wanachuoni waekubaliana juu ya kwamba kumtuhumu machafu mwanaume ambaye ametakasika ni kama kumtuhumu machafu mwanamke ambaye ametakasika. Kwa sababu Kimsingi ni kuwa wanaume na wanawake ni sawa katika hukumu za Allaah (Ta´ala).

[1] 24:04-05

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (36) http://binothaimeen.net/content/796
  • Imechapishwa: 22/01/2018