Mwanamke ametwahirika katikati ya mchana wa Ramadhaan


Swali: Umeashiria tofauti iliopo kwa mwanamke aliyesafika kipindi cha mchana kutokamana na hedhi au damu ya uzazi kama analazimika kujizuia siku iliyobaki au halazimiki. Wale wanaosema kuwa ni lazima kwake kujizuia siku iliyobaki wanajengea hoja kwamba wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipowajibisha kufunga siku ya ´Aashuuraa alimwamrisha yule ambaye amekula baada ya kupambazuka kujizuia.  Je, dalili yao ni sahihi?

Jibu: Nimesema juu ya mwanamke kama alikuwa na hedhi na akasafika katikati ya mchana wa Ramadhaan, kwamba wanazuoni wametofautiana kama analazimika kujizuia kutokamana na kula na kunywa siku iliyobaki au halazimiki. Nilisema kuwa Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) ana mapokezi mawili juu ya maudhui hayo. Moja wapo ambayo imetangaa sana katika madhehebu ni kwamba analazimika kujizuia siku iliyobaki. Maoni ya pili yanasema kuwa si lazima kwake kujizuia na hivyo inafaa kwake kula na kunywa. Aidha tukasema kuwa haya maoni ya pili ndio ya madhehebu ya Maalik na ash-Shaafi´iy (Rahimahumaa Allaah) na kwamba Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Ambaye amekula mwanzoni mwa mchana basi ale vilevile mwishoni mwake.”

Aidha nikasema kuwa ni lazima kwa mwanafunzi juu ya mambo ya tofauti daima atafiti dalili, atendee kazi yale ambayo ataona kuwa ni yenye nguvu na kwamba asijali yale watayoonelea wengine muda wa kuwa ameshikamana na dalili. Sisi tumeamrishwa kuwafuata Mitume:

يَوْمَ يُنَادِيهِمْ فَيَقُولُ مَاذَا أَجَبْتُمُ الْمُرْسَلِينَ

”Siku atakapowaita aseme: “Mliwajibu nini Mitume?”[1]

Kuhusu kule kujengea kwao hoja kwa Hadiyth, hawana mashiko yoyote. Kwani Hadiyth haina kuondosha kizuizi chochote isipokuwa kufanya upya jambo la wajibu. Kwa sababu kufanya upya jambo la wajibu hiyo ina maana kwamba hukumu hiyo haikuweko kabla ya kuwepo sababu yake, ama kuondoka kwa kikwazo hiyo ina maana kwamba hukumu ilikuweko kabla ya kuondoka kizuizi; lau si kuweko kwa kizuizi hiki basi hukumu ingeendelea. Mfano wa hali hiyo ni kama mtu ambaye anasilimu kipindi cha mchana wa Ramadhaan; uwajibu wake umekuwa mpya. Tunamwambia mtu huyo kwamba ni lazima kwake kujizuia siku iliyobaki, lakini halazimiki kuilipa siku hiyo. Vivyo hivyo mtoto ambaye anabalaghe kipindi cha mchana wa Ramadhaan; uwajibu wake umekuwa mpya. Mtoto huyu ni lazima kwake kujizuia siku iliyobaki, lakini halazimiki kuilipa siku hiyo. Hali hizo ni tofauti na mwanamke mwenye hedhi anapotwahirika katikati ya mchana. Wanazuoni wote wameafikiana kuwa ni lazima kwake kuilipa siku hiyo. Wanazuoni wote pia wameafikiana kwamba mwanamke anayesafika kipindi cha mchana wa Ramadhaan na hivyo akajizuia siku iliyobaki, hakumnufaishi kitu kujizuia huko, na wala haizingatiwi kuwa ni swawm iliyowekwa katika Shari´ah na kwamba analazimika kuilipa siku hiyo. Kwa njia hiyo tumepata kufahamu tofauti ya wajibu kuwa mpya na kuondokewa na kizuizi. Mwanamke mwenye hedhi anapotwahirika katikati ya Ramadhaan ni kuzuizi ndio kimemwondoka. Mtoto ambaye anabaleghe katikati ya mchana wa Ramadhaan na hiyo Haidyth uliyotaja ya ´Aashuuraa inahusiana na wajibu kuwa mpya.

[1] 28:65

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (19/100-102)
  • Imechapishwa: 05/05/2021