Mwanafunzi kubeba viatu vya mwalimu

Tunajua kuwa walikuweko Maswahabah ambao walikuwa wanatambulika kubeba makubadhi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Je, unaona kuwa mwanafunzi anatakiwa kufanya hivo kwa yule mwalimu wake anayempenda? Je, tumwache afanye hivo? Sionelei hivo. Kwa nini? Mfano wa maadhimisho haya yanaweza kuwa mtihani kwa yule mfataji na mfuatwaji. Kwa ajili hiyo ni munasibu kumnukuu Abu ´Umar bin ´Abdil-Barr ambaye amesema:

“Kubusu mikono ni Sujuud ndogo.”

Kuna mwingine ima yeye au mwingine, shaka hiyo ni kutoka kwangu, ambaye amesema:

“Kubusu mikono ni mtihani kwa mfuatwaji na ni udhalilifu kwa yule mfataji.”

Hili wakati mwingine linaweza kuonekana pindi mtu anabusu mkono wa mwalimu na akamuinamia. Kuinama ni aina fulani ya Sujuud. Hayo yanajulishwa na Hadiyth ya Mu´aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ´anh); alikuwa ameenda kutembea Dameski wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akawa mbali naye kwa kipindi cha masiku kadhaa. Hapana shaka kwamba kipindi cha kuwa kwake mbali hichi alikuwa na shauku kubwa juu ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Pale tu alipomuona Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akataka kumsujudia. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamkataza na akamuuliza ni nini anachotaka kufanya. Mu´aadh akasema:

“Ee Mtume wa Allaah! Mimi nimefika Shaam na nikawaona manaswara wanawasujudia makasisi wao na watawa wao; ndipo nikaona kuwa wewe una haki zaidi ya kufanyiwa Sujuud kuliko wao.”

Alitaka kumuadhimisha kwa matukuzo na heshima, lakini kufanya hivo sio kuadhimisha. Hili ni baya zaidi kuliko kusimama kwa ajili yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ninachotaka kusema ni kwamba kama mwalimu angelikuwa mkamilifu kama Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mwalimu angelikuwa kama Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh), basi ningeonelea kuwa inafaa kwake kubeba makubadhi ya mwalimu wake. Katika hali hiyo nisingechelea mtihani kwa yule mfuatwaji wala udhalilifu kwa yule mfataji. Kwa ajili hiyo siwezi kusema kwamba wanafunzi hii leo wanatakiwa kuwaheshimu wanazuoni wao kama ambavo Maswahabah walivokuwa wakimuheshimu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini kama nilivotangulia kusema mtu anatakiwa kufanya kadri na anavoweza.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Hudaa wan-Nuur (1010)
  • Imechapishwa: 21/06/2021