Musw´ab bin ´Umayr


Alikuwa anaitwa Musw´ab bin ´Umayr bin Haashim bin ´Abd Manaaf bin ´Abdid-Daar bin Qusayy bin Kilaab al-Badriy, al-Qurashiy, al-´Abdariy. Alikuwa ni bwana, shahidi na mmoja katika wale wanamme waliotangulia mwanzonimwanzoni.

al-Baraa´ bin ´Aazib amesema:

”Mtu wa kwanza aliyetujia [al-Madiynah] katika Muhaajiruun alikuwa ni Musw´ab bin ´Umayr. Tukamuuliza: ”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa slalam) anafanya nini?” Akajibu: ”Yuko mahala pake na Maswahabah zake wanafuata nyayo zangu.” Kisha baada yake akaja kipofu ´Amr bin Umm Maktuum.”[1]

Khabbaab amesema:

“Tulihajiri pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika njia ya Allaah tukitafuta uso wa Allaah ambapo ikawajibika ujira wetu kwa Allaah. Miongoni mwetu ambao wamekwishakupita hawakula chochote kutoka katika ujira wao. Mmoja wa watu hao ni Musw´ab bin ´Umayr ambaye aliuawa siku ya Uhud na hakujapatikana kwake chochote isipokuwa nguo moja tu. Tulikuwa tunapoiweka kichwani mwake basi miguu yake inabaki wazi na tunapoiweka miguu mwake basi kichwa chake kinabaki wazi. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Mfunikeni kwayo kichwa chake na wekeni juu ya miguu yake majani ya al-Idhkhira[2]. Miongoni mwetu wako wale ambao matunda yao yalikuwa yamekwishawiza na wako tayari kuyavuna.”[3]

Shu´bah amepokea kutoka kwa Sa´d bin Ibraahiym ambaye amemsikia baba yake akisema:

“Chakula kililetwa mbele ya ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf. Akaanza kulia na kusema: “Hamzah ameuliwa na hakukupatikana kitu cha kumfunika isipokuwa shuka moja. Musw´ab ameuliwa na hakukupatikana kitu cha kumfunika isipokuwa shuka moja. Nachelea tumeharakishiwa kuburudika kwetu katika maisha haya ya dunia.” Kisha akawa analia.”[4]

Ibn Ishaaq amesema:

“Musw´ab bin ´Umayr alipambana mbele ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa slalam) mpaka alipouliwa. Aliuliwa na Qami´ah al-Laythiy ambaye alikuwa anafikiri kuwa ndiye Mtume wa Allaah. Akarejea kwa Quraysh na kusema:

“Nimemuua Muhammad.”

Wakati alipouliwa Musw´ab, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa slalam) alimpa bendera ´Aliy bin Abiy Twaalib na wanamme wengine katika waislamu.”[5]

[1] al-Bukhaariy (3924).

[2] Ni majani yanayojulikana yenye harufu nzuri.

[3] al-Bukhaariy (1286).

[4] al-Bukhaariy (1274).

[5] Tazama Ibn Hishaam (2/73), Ibn Sa´d (3/1/85) na al-Istiy´aab (10/251).

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Siyar A´laam-in-Nubalaa' (1/145-148)
  • Imechapishwa: 08/03/2021