Swali: Mwanamke analalamika juu ya mume wake ambaye haswali wala hafungi kabisa. Mume ana maono juu yake yasiyokuwa mazuri na anamlazimisha kula katika Ramadhaan. Ni ipi hukumu ya kubaki pamoja naye? Ni kipi kinachomlazimu kufanya kama amelazimishwa kufungua?

Jibu: Ni jambo linalosikitisha kuona watu kama hawa wako nchini mwetu, nchi ambayo ni ya Kiislamu na iliyohifadhiwa. Nchi ambayo Allaah ameitunuku raha na amani, neema mbili ambazo inatakiwa kuzikabili kwa shukurani na kuzidisha utiifu. Lakini kwa masikitiko makubwa ni kwamba baadhi ya watu neema haziwazidishii jengine isipokuwa dhuluma, uovu na ubaya.

Bwana huyu ambaye haswali wala hafungi hapana shaka naonelea kuwa ni kafiri na mritadi. Hiyo ina maana kwamba ndoa yake imefutika. Si halali kwake mwanamke huyu kubaki akaishi naye kwa muda wa kupepesa macho, kwa sababu ndoa yake imefutika kwa kule kuritadi kwake. Ni lazima kwa mke wake kwenda nyumbani kwa familia yake na kuachana naye. Allaah akimwongoza kabla ya kumalizika kwa eda, basi bado ataendelea kuwa mke wake. Eda yake ikimalizika kabla ya kurudi katika Uislamu, basi wanazuoni wengi wanaona kuwa mwanamke huyo hawezi kumrejea mpaka asilimu upya na wafungishwe ndoa upya. Wanazuoni wengine wanaona kuwa anaweza kumrejelea bila kufunga ndoa upya. Kwa hiyo mwanamke anakuwa na uamuzi baada ya kutubia akitaka atarudi kwa mwanaume huyo na asipotaka hatorudi kwake. Haya ndio maoni ya sawa.

Ama kitendo cha kumlazimisha yeye kufungua, kama alilazimishwa na akashindwa kumzuia basi hakuna chochote kinachomlazimu. Hata hivyo huko mbele ahakikishe amerudi nyumbani kwao na amejikwamua naye.

  • Mhusika: Imâm Muhammad bin Sâlih bin ´Uthaymîn (d. 1421)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (19/276-277)
  • Imechapishwa: 04/05/2021