Muislamu anatakiwa kujitahidi katika zile siku kumi za mwisho


Swali: Ni zipi alama za Laylat-ul-Qadr? Ni yepi ya wajibu kwa muislamu katika usiku huo?

Jibu: Sunnah ni mtu kusimama usiku wa makadirio. Usiku huo unapatikana katika zile siku kumi za mwisho za Ramadhaan. Siku zisizogawanyika ndio zenye kukokotezwa zaidi kuliko zengine. Usiku wenye nguvu zaidi ni usiku wa tarehe ishirini na saba.

Kilichowekwa katika Shari´ah ni mtu kujitahidi katika kumtii Allaah (´Azza wa Jall) katika michana yake na nyusiku zake. Kusimama nyusiku si kwamba ni jambo la wajibu. Bali ni jambo lililopendekezwa. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akijitahidi katika zile siku kumi za mwisho kuliko anavojitahidi katika masiku mengine. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yalipokuwa yanaingia yale masiku kumi ya mwisho basi hukaza kikoi chake, anauhuisha usiku wake na anawaamsha wake zake.”[1]

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule atakayesimama usiku wa makadirio kwa imani na kwa matarajio, basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”[2]

Kuna Hadiyth nyingi kuhusu hilo.

[1] al-Bukhaariy (1884) na Muslim (2008).

[2] al-Bukhaariy (1768) na Muslim (1268).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (15/431-432)
  • Imechapishwa: 09/06/2018