Swali: Mkazi ana muda kiasi gani wa kupangusa juu ya khofu mbili?

Jibu: Muda wake ni mchana na usiku mmoja. Kwa msemo mwingine masaa ishirini na nne. Muda huu unaanza kuanzia mpanguso wa kwanza aliopangusa. Hapo ndipo ataanza kuhesabu mpaka siku ya pili. Kwa mfano kama ameanza kufuta saa kumi na mbili kamili ya leo basi ataendelea kupangusa mpaka saa kumi na mbili ya siku inayofuata. Akifuta kabla ya muda kuisha na akabaki akiwa na twahara yake na muda ukamuishia hali ya kuwa bado yuko na twahara yake, basi wudhuu´ wake hauchenguki. Atabaki akiwa na wudhuu´ wake mpaka uchenguke kwa kichenguzi kinachotambulika.

Swali: Kwa hiyo ina maana kwamba hatohesabu muda wa kabla ya kufuta. Kwa mfano ametawadha Fajr na akaendelea kuwa na wudhuu´ wake mpaka Dhuhr, ´Aswr na Maghrib kisha akatawadha [kwa kufuta] wakati wa ´Ishaa. Ataanza kuhesabu muda kuanzia wakati huu wa ´Ishaa ya leo mpaka ´Ishaa ya kesho kwa muda wa masaa ishirini na nne?

Jibu: Ndio. Nakwambia kitu kingine: tukadirie kuwa ameswali ´Ishaa kwa wudhuu´ wa Fajr ya jana na akaanza kupangusa Fajr ya siku ya pili, basi muda atahesabu kuanzia Fajr ya siku hii ya pili. Tukadirie pia kuwa siku ya tatu amewahi kupangusa kabla ya kuisha muda wa kupangusa na akabaki na wudhuu´ wake mpaka wakati wa ´Ishaa siku ya tatu au ya nne, kitendo hicho ni sahihi pia. Kwa ajili hiyo baadhi ya wasiokuwa wasomi wanakosea pale wanaposema kwamba mwenye kuvaa soksi basi inafaa kwake kuswali vipindi vitano. Sivyo. Kuna uwezekano akaswali zaidi ya vipindi vitano.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb (17) http://binothaimeen.net/content/6817
  • Imechapishwa: 15/03/2021