Muadhini ana haki ya adhaana na imamu ana haki ya Iqaamah

Swali: Imamu alichelewa kidogo ambapo muadhini akawa ameadhini kwa ajili ya swalah na akawaswalisha watu. Imamu mteule akaja na akaingia kwenye Mihrab na akaanza swalah na baadhi ya watu wakawa wamemfuata na waswaliji wengine wakabaki katika ile Takbiyr yao ya kwanza. Ni yapi maoni yako?

Jibu: Muadhini alienda wapi? Namaanisha kweli muadhini alienda wapi? Kumekuwa maimamu wawili katika msikiti mmoja! Kwa hali yoyote Iqaamah ni jukumu la imamu na adhaana ni jukumu la muadhini. Muadhini hana haki ya kukimu swalah mpaka aje imamu mteule. Akifanya hivo anapata dhambi. Waswaliji pia wakiona kuwa muadhini anataka kukimu swalah kabla ya kutokea imamu mteule wamkataze. Kwa sababu Iqaamah ni haki ya imamu.

Lakini endapo imamu atachelewa na nyumbani kwake kukawa ni karibu, basi wanachuoni wanasema kwamba aendewe. Hivyo ndivyo walivyokuwa wakifanya Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anapochelewa wanamwendea na kumwambia kuwa sasa ni wakati wa swalah. Ama nyumbani kwake ikiwa ni mbali basi ni wenye kupewa udhuru. Hapa ni pale ambapo imamu atachelewa uchelewaji ambao sio wa kawaida kidesturi.

Lakini mimi nasema ikiwa imamu kwa mfano ana shughuli au kazi na anachelea asije kuchelewa swalah ya Dhuhr, basi awaambie kwamba endapo atachelewa, kama mfano wa dakika 10, basi wakimu swalah. Katika hali hiyo kunakuwa na raha kwake na kwa wao. Akija na akawakuta wanaswali basi atajiunga pamoja nao. Hivyo ndivyo alivyofanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku moja alipokuja amechelewa na alikuwa anaenda kwa Banuu ´Awf kufanya suluhu, akawakuta watu wanaswalishwa na ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf (Radhiya Allaahu ´anh) ambapo akawa amejiunga pamoja nao katika swalah. Akawa maamuma (´alayahis-Swalaatu was-Salaam).  Hakuna ubaya. Haina maana kwamba imamu akiwa maamuma – kama ilivyo katika hali hii – anakuwa ni mwenye kuchukiwa.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (40) http://binothaimeen.net/content/906
  • Imechapishwa: 25/09/2018