Mtu kusimulia dhambi aliyoifanya baada ya Allaah kumsitiri

Swali: Mtu akifanya dhambi mwanzoni mwa uhai wake na Allaah akamsitiri na asijue yeyote isipokuwa Allaah pekee (´Azza wa Jall). Baada ya hapo Allaah akamruzuku tawbah na akatubu. Je, inafaa kwake kuwafundisha watu dhambi hiyo aliyoifanya mwanzoni mwa uhai wake au hapana? Pamoja na kuzingatia kwamba baadhi ya watu wanamlazimisha Allaah awafunze yale waliyoyatenda katika maisha yao na kwamba mwenye kutangaza dhambi zake basi Allaah anamsamehe. Je, maneno haya ni sahihi?

Jibu: Swali hili ndani yake kuna maswali matatu:

1- Inafaa kwa mtu ambaye amefanya dhambi na Allaah akamsitiri kuwaeleza wengine? Jibu ni kwamba haifai kwa ambaye amefanya dhambi na Allaah akamsitiri kuwaeleza wengine. Kwa sababu kufanya hivo ni kufunua sitara ya Allaah (´Azza wa Jall). Ni kwenda kinyume na msamaha. Imekuja katika Hadiyth:

“Ummah wangu wote ni wenye kusamehewa isipokuwa wenye kudhihirisha [madhambi].”

Hao ni wale wanaofanya madhambi kisha wanasimulia waliyoyafanya. Ikiwa dhambi inapelekea katika kuadhibiwa na mtu akataka kumweleza mtawala ili amsafishe na dhambi au adhabu hii, katika hali hii hakuna neno ingawa bora zaidi ni yeye kujisitiri kwa sitara ya Allaah. Ama dhambi ikiwa sio aina hii haifai kwa mtu akaieleza mbele za watu. Kufanya hivo ni kujidhulumu nafsi yake, kufungua mlango juu ya wengine kuichukulia si lolote si chochote.

Kuhusu kuwaomba wengine wamjulishe dhambi walizofanya, haifai kwa mtu kuwatia uzito wengine kwa kuwauliza maswali kama haya. Kufanya hivi ni kwenda kinyume na Uislamu mzuri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Katika Uislamu mzuri wa mtu ni kuyaacha mambo yasiyomuhusu.”

Katika hali kama hii huhitajii kumjibu hata kama atakuomba kwa jina la Allaah (´Azza wa Jall). Si lazima kwako kumjibu katika jambo hili. Kwani jambo hili lina madhara kwako na ni kukudhulumu. Allaah hawapendi madhalimu na wala hapendi dhuluma. Haijuzu kwako kukuuliza swali kama hili.

Mwenda kipindi: Vipi kuhusu kwamba mwenye kuwaeleza wengine madhambi aliyoyafanya basi Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) anamsamehe siku ya Qiyaamah?

Jibu: Hili si sahihi. Tumetangulia kusema kwamba haifai kwa mtu kuwaeleza wengine dhambi alizofanya. Allaah anasamehe mtu pale anapotubia Kwake, akarejea Kwake kuacha dhambi yake, akajutia, akaazimia kutorudi kufanya hivo katika mustakabali na tawbah ikawa kwa wakati wake. Kwa msemo mwingine tawbah ikawa kabla ya mtu kufikwa na kifo na kabla ya jua kuchomoza kutoka magharibi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb (14) http://binothaimeen.net/content/6784
  • Imechapishwa: 10/02/2021