Mtu kujisafisha tupu baada ya kutokwa na pumzi

Swali: Ni wajibu kwa mtu kujiosha na maji anapotokwa na pumzi?

Jibu: Kutokwa na pumzi kwenye tupu ya nyuma kunachengua wudhuu´. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Asitoke [ndani ya swalah] mpaka ataposikia sauti au atahisi harufu yake.”

Lakini hata hivyo hakuwajibishi kuosha tupu kwa maji. Hakukutoka kitu kinachopelekea kuosha.

Kujengea juu ya hili mtu anapotokwa na pumzi wudhuu´ wake unachenguka. Inatosha kwa mtu kutawadha; kuosha uso wake, kusukutua, kupalizia, mikono yake mpaka kwenye visugudi, apanguse kichwa chake, masikio yake na aoshe miguu yake mpaka kwenye vifundo vya miguu.

Hapa napenda kuzindua jambo ambalo limefichikana kwa watu wengi. Balo ni kwamba baadhi ya watu wanajisaidia haja ndogo au kubwa katika wakati usiokuwa wa swalah kisha wanajisafisha kwa maji. Inapofika wakati wa swalah na akataka kutawadha, wapo watu wanaodhani kuwa ni lazima kurudi kuisafisha tupu kwa mara ya pili. Hili si sawa. Mtu anapoiosha tupu yake baada ya kutokwa na kitu basi sehemu hiyo imesafika. Kama ameshasafika basi hakuna haja ya kurudi kuosha kwa mara nyingine. Kwa sababu malengo ya kujisafisha kwa maji au kwa mawe kwa mujibu wa masharti yake yanayotambulika ni kusafisha sehemu. Pakisafika basi harudi kwenye najisi hiyo isipokuwa ikiwa kama najisi itatoka tena upya kwa mara nyingine.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (11/112-113)
  • Imechapishwa: 14/06/2017