Mtazame yule aliye chini yenu na wala msimtazame aliye juu yenu

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mtazame yule aliye chini yenu na wala msimtazame aliye juu yenu. Kwani [kufanya hivo] ni haki zaidi msije mkazidharau neema za Allaah juu yenu.”[1]

Ameelekeza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika dawa hii ya ajabu na sababu yenye nguvu ya kuzishukuru neema za Allaah. Mtu anatakiwa kila wakati kumzingatia yule aliye chini yake katika akili, ukoo, mali na neema mbalimbali. Pale ambapo atakuwa na mtazamo huo basi itamlazimu kumshukuru Mola wake na kumsifu. Hakika siku zote ataendelea kuwaona viumbe wengi walio chini yake kwa daraja mbalimbali juu ya sifa hizi na wengi katika watu hao nao wanatamani kufika karibu na yale aliyopewa yeye katika afya njema, mali, riziki, maumbile na tabia. Kwa hivyo amshukuru Allaah kwa hayo shukurani nyingi na aseme:

الحمد لله الذي أنعم عليَّ وفضلني على كثير ممن خلق تفضيلاً

“Himdi zote njema anastahiki Allaah ambaye amenineemsha na akanifadhilisha daraja nyingi juu ya wengi aliyowaumba.”

Awatazame viumbe wengi waliopokonywa akili zao na hivyo amshukuru Mola wake juu ya utimilifu wa akili. Awatazame viumbe wengi wasiokuwa na chakula cha kuweka akiba wala makazi ya kuwalinda ilihali yeye ametulizana ndani ya makazi yake na amepanuliwa riziki yake.

Upande wa pili anawaona viumbe wengi waliopewa mtihani kwa maradhi na magonjwa aina mbalimbali ilihali yeye amelindwa kutokamana na hayo na ni mwenye afya njema. Vilevile anawaona viumbe wengi waliopewa mtihani mkubwa kuliko huo ambao ni kupotea katika dini na kutumbukia katika uchafu wa maasi ilihali yeye Allaah amemlinda kutokamana na hayo au mengi katika hayo.

[1] Muslim (2963), at-Tirmidhiy (2513), na Ahmad (02/254).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bahjatu Quluub-il-Abraar, uk. 54-55
  • Imechapishwa: 04/02/2020