Imaam at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Miguu ya Uislamu haiwi imara isipokuwa kwa ujisalimishaji wa wazi na kujisalimisha.”

Miguu ya Uislamu haithibiti isipokuwa kwa kujisalimisha na maandiko ya Qur-aan na Sunnah na kunyenyekea kwayo na asipingane nayo kwa kuleta maoni yake, akili zake na kipimo chake. Imaam Muhammad bin Shihaab az-Zuhriy amesema kutokana na yale al-Bukhaariy alipokea kutoka kwake:

“Ujumbe ni wenye kutoka kwa Allaah, ni juu ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kufikisha na lililo juu yetu ni kujisalimisha nayo.” “Fath-ul-Baariy” (13/503) al-Bukhaariy.

Haya ni maneno ya jumla na yenye manufaa.

Hakuna njia ya mja kuokoka isipokuwa kwa kumpwekesha Allaah (´Azza wa Jall) na kumfuata Mtume peke yake. Ni mambo mawili ambayo mja hawezi kuokoka isipokuwa kwa kuyaleta yote mawili. Mja hawezi kuokoka kutokana na adhabu ya Allaah isipokuwa kwa upwekeshaji aina mbili huu:

1- Ampwekeshe Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

2- Amfuate Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) peke yake.

Tunajipwekesha kwa Allaah kwa kumuabudu, kunyenyekea Kwake, kujidhalilisha Kwake, kurejea Kwake na kumtegemea Yeye.

Kadhalika tunampwekesha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa kuhukumiwa na yeye peke yake na si kwa mwingine. Haturidhii hukumu ya mwingine. Tunanyenyekea amri yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na tunakubali maelezo yake kwa kuyapokea na kuyasadikisha bila ya kupingana nayo kwa fikira mbovu ambazo tunaita kuwa ni “akili” au tukayatilia utata au shaka au tukayatangulizia juu yake maoni na makosa ya wanaume au tukasimama kutekeleza maamrisho yake na kusadikisha maelezo yake. Badala yake tukapingana nayo kwa sababu ya maneno ya Shaykh au Imaam au madhehebu au pote fulani. Wakiyapitisha na sisi tunayapitisha na wakiyakataa na sisi tunayatupilia mbali. Haya yanafanywa na wale ambao hawakujisalimisha na maandiko ya Qur-aan na Sunnah. Lililo la wajibu ni kuhukumiana, kujisalimisha na kunyenyekea kwayo.

Akili ya wazi haiwezi kupingana na andiko sahihi. Yale ambayo Shari´ah imeleta ni yenye kuafikiana na akili ilio sahihi. Andiko sahihi kamwe haliwezi kwenda kinyume na akili ya wazi. Vikipingana pamoja na kwamba andiko ni sahihi, basi huyo anayejidai kuwa ana akili nyingi ni lazima akili zake ziwe hazikutimia na bali naweza kusema kuwa ni mjinga. Lau atatafakari vizuri basi atakuja kugundua hilo. Ama ikiwa andiko sio sahihi, si sawa kupingana na kilicho asli [akili].

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hidaayah ar-Rabbaaniyyah fiy Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (01/269)
  • Imechapishwa: 23/05/2020