24. Msimamo wa sawa juu ya Aayah kuhusu sifa na majina ya Allaah

Imaam al-Barbahaariy (Rahimahu Allaah) amesema:

Hakuzungumzwi juu ya Allaah isipokuwa kwa yale aliyojisifu Mwenyewe katika Qur-aan na yale Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyowabainishia Maswahabah zake. Hakika Yeye (Jalla Thanaa´uh) ni Mmoja:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (42:11)

MAELEZO

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ni Mmoja na hashirikiani na yeyote, si katika Dhati Yake, majina na sifa Zake wala viumbe Vyake. Ni Mmoja (Jalla wa ´Alaa) asiyekuwa na mshirika. Kwa nini basi unaitaabisha nafsi yako? Wewe ni kiumbe na Yeye ndiye Muumba. Vipi basi kiumbe ataweza kumjua kwa kumzunguka Muumba (Jalla wa ´Alaa)? Huna juu yako isipokuwa kujisalimisha kwa Allaah (Ta´ala) na kwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Usijadili wala kuleta ushindani na wala usiitaabishe nafsi yako na ukataabisha wengine. Hili ndilo la wajibu.

Kwa ajili hiyo Maswahabah hawakujikalifisha makalifisho yote haya na wala hawakusimama katika Aayah hata moja wala Hadiyth. Uhakika wa mambo walikuwa wakisoma na kujisalimisha kwayo na kuitakadi yaliyomo na wala hawakuwa na migogoro kamwe. Hakuna jengine katika nafasi hii isipokuwa kujisalimisha tu.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Sharh-is-Sunnah, uk. 59-60
  • Imechapishwa: 08/01/2018