Msimamo wa Muislamu kwa jirani yake ambaye ni kafiri

Swali: Mimi nina jirani mnaswara ambaye nimemlingania katika Uislamu mara nyingi lakini hata hivyo amekataa na kuendelea kubaki katika unaswara na kwamba dini yake ndio ya haki. Je, napata dhambi kuzungumza na kutangamana nae? Ni lipi la wajibu kuhusiana na yeye?

Jibu: Kila kinacholeta mapenzi kati ya muislamu na kafiri basi ni njia inayopelekea katika mapenzi. Allaah (Ta´ala) amesema:

لَّا تَجِدُ قَوْمًا يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ يُوَادُّونَ مَنْ حَادَّ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ

”Hutopata watu wanaomuamini Allaah na siku ya Mwisho kuwa wanawapenda wanaompinga Allaah na Mtume Wake.”[1]

Haifai kwa mtu kufanya kitu kinachopelekea katika mapenzi. Akijaribu kufanya hivo basi amejaribu katika kufanya kitu ambacho kitamuondoshea imani yake ima uondoshaji wa moja kwa moja au wa kikamilifu. Lakini kafiri akitusalimia na sisi tunamsalimia. Hatufanyi vibaya ujirani wake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Yule mwenye kumuamini Allaah na siku ya Mwisho basi amkirimu jirani wake.”

Wanachuoni wamesema kuna majirani aina nne:

Ya kwanza: Kuna jirani ambaye ni ndugu na wakati huohuo ni muslamu. Huyu ana haki tatu:

1- Haki ya ujirani.

2- Haki ya udugu.

3- Haki ya Uislamu.

Ya pili: Jirani ambaye ni ndugu na ni kafiri. Huyu ana haki mbili:

1- Haki ya ujirani.

2- Haki ya udugu.

Ya tatu: Jirani ambaye ni muislamu lakini sio ndugu. Huyu ana haki mbili pia:

1- Haki ya ujirani.

2- Haki ya Uislamu.

Ya nne: Jirani ambaye ni kafiri. Huyu ana haki moja:

1- Haki ya ujirani.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Yule mwenye kumuamini Allaah na siku ya Mwisho basi amkirimu jirani wake.”

Kumkirimu haina maana kwamba umpende. Mara nyingi mtu anaweza kumkirimu mtu kama mgeni aliyemjia, mtu amekutana na mwenzie katika safari, anamkirimu na kumtukuza na huenda hata akamfanyia chakula na wakati huohuo hampendi. Mapenzi na kila kile kinachopelekea katika mapenzi kati ya muislamu na kafiri ndicho ambacho kinafanya imani kupungua.

[1] 58:22

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (30) http://binothaimeen.net/content/679
  • Imechapishwa: 10/10/2017