Ikiwa mwandishi al-Khaliyliy anathibitisha kuwa Ibaadhiyyah wanafuata mfumo wa Abu Hamzah al-Mukhtaar na kwamba ndio mfumo uliosalimika. Kama tulivyoona katika mfumo huo ni kwamba wanaonelea mshirikina ambaye anaabudu mzimu, kafiri ambaye ni myahudi au mnaswara na mtawala dhalimu wa Kiislamu wako sambamba kihukumu na kwamba wanajitenga mbali na wote hao.

Tunamuuliza al-Khaliyliy msimamo wake juu ya dalili zilizothibiti kutoka katika Sunnah ambazo umesema juu yake kwamba kurejea kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuna maana nyingine isipokuwa kurudi katika Sunnah zilizothibiti na Swahiyh. Je, wewe hukubali kwamba yale yaliyopokea al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Swahiyh? Mambo yakiwa ni hivo – na sidhani kuwa unakhalifu hilo – unasemaje juu ya Hadiyth zinazokuja hapa mbele ambazo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anawazungumzia watawala madhalimu na kwamba wanatakiwa kusikilizwa na kutiiwa katika mema na kutofanya uasi dhidi yao?

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea:

“Ni juu ya muislamu kusikiliza na kutii katika yale anayoyapenda na kuyaridhia isipokuwa tu pale atapoamrishwa maasi. Akiamrishwa maasi hakuna kusikiliza wala kutii.”[1]

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea tena kupitia kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) aliyesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atayeona kutoka kwa mtawala wake kitu anachokichukia asubiri. Atayefarikiana na mkusanyiko (Jamaa´ah) shibri moja na akafa, basi kifo chake kitakuwa ni cha kipindi cha kishirikina.”[2]

Muslim amepokea kupitia kwa ´Awf bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Watawala wenu bora ni wale mnaowapenda na wao wanakupendeni na mnawaombea na wao wanakuombeeni. Watawala wenu waovu ni wale mnaowachukia na wao wanakuchukieni na mnawalaani na wao wanakulaanini.” Tukasema: “Ee Mtume wa Allaah! Itapofikia kuwa hivo tusipambane nao kwa upanga?” Akasema: “Hapana, maadamu wanaswali. Tanabahini! Atayetawaliwa na mtawala na akaona anafanya kitu katika kumuasi Allaah, basi atachukie kile anachofanya katika kumuasi Allaah na wala asiondoe mkono wake kutoa katika utiifu.”[3]

Kuna Hadiyth nyingi zilizo na maana kama hiyo.

Haya ndio maamrisho ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba inatakiwa kuwatii watawala hata kama watafanya ukandamizaji na maasi. Madhambi yako kwako.

Hata hivyo ni wajibu kuwanasihi, kuwaelekeza, kuwakumbusha na kuwaombea du´aa ya kutengamaa. Kwani kuwafanyia uasi kunapelelea katika madhara mengi kukiwemo kumwagika damu na heshima za watu kuvunjwa mara dufu kuliko ule udhalimu wanaofanya. Kwa ajili hii ndio maana Sunnah imesisitiza sana juu ya kulazimiana na kuwatii hata kama watafanya ukandamizi. Isipokuwa tu pale watapofanya kufuru ya wazi ambayo kuna dalili kwayo kutoka kwa Allaah na wakati huo huo kukawa kuna uwezo wa kumg´oa pasi na kusababisha madhara makubwa zaidi kuliko ukandamizaji wao.

[1] al-Bukhaariy (7144) na Muslim (1839).

[2] al-Bukhaariy (7143) na Muslim (1849).

[3] Muslim (1855).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Aliy bin Naaswir al-Faqiyhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ar-Radd al-Qawiym, uk. 21-23
  • Imechapishwa: 13/01/2017