Msemo “Ramadhaan Kariym” kwa mtazamo wa Ibn ´Uthaymiyn


Swali: Pindi mfungaji anapotumbukia katika maasi na akakumbushwa, anasema kuwa Ramadhaan ni karimu. Ni ipi hukumu juu ya hilo?

Jibu: Si sahihi kusema hivo. Mtu anatakiwa kusema Ramadhaan yenye baraka (Ramadhaan Mubaarak) na mfano wake. Si Ramadhana yenye kutoa mpaka iwe karimu. Allaah (Ta´ala) ndiye Mwenye kutoa na ndiye kaifanya Ramadhaan kuwa ni mwezi wenye fadhilah ambapo mtu anatekeleza nguzo ya Uislamu.

Ni kama kwamba huyu anadhani kuwa inafaa kufanya maasi ndani ya mwezi huu kwa sababu tu ni mwezi mtukufu kwa mwaka. Hili ni kinyume na vile walivosema wanachuoni kwamba madhambi yanakuwa ya khatari kutokana na utukufu wa maeneo na wakati. Wanasema kuwa ni wajibu kwa mtu kumcha Allaah (´Azza wa Jall) pasi na kujali wakati na maeneo. Hili khaswa khaswa katika nyakati tukufu na maeneo matukufu. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Enyi walioamini! Mmefaridhishwa funga kama ilivyofaridhishwa kwa walio kabla yenu mpate kuwa na kucha.” (02:183)

Lengo la kufaradhishwa swawm ni kumcha Allaah (´Azza wa Jall) kwa kutekeleza maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake. Imethibiti ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule asiyeacha maneno ya uongo, kuutendea kazi na ujinga, basi Allaah hana haja kwa yeye kuacha chakula na kinywaji chake.”[1]

Swawm ni ´ibaadah inayoilea nafsi na kuilinda kutokamana na yale aliyoharamisha Allaah. Sivyo kama alivosema mjinga huyu na kuashiria kwamba inafaa kufanya maasi ndani ya mwezi huu kutokana na utukufu na baraka za mwezi huu.

[1] al-Bukhaariy (1903).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://www.sahab.net/forums/index.php?app=forums&module=forums&controller=topic&id=130714
  • Imechapishwa: 20/05/2018