Msamaha wa Allaah unawahusu watenda dhambi wa sampuli hii

Imaam at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Wenye madhambi makubwa katika Ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hawatodumishwa Motoni milele endapo watakufa hali ya kuwa ni wapwekeshaji hata kama watakuwa hawakutubu.”

Kwa kupatikana kigezo hiki: ni lazima aliyetenda dhambi kubwa awe amekufa juu ya Tawhiyd. Ama ikiwa amekufa juu ya shirki, basi huyu amefungiwa mlango wa Rahmah. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa.” (04:48)

Pepo kwake ni haramu kama alivosema (Subhaanah):

إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ

“Hakika mwenye kumshirikisha Allaah bila shaka Allaah atamharamishia Pepo na makazi yake yatakuwa ni Motoni.” (05:72)

Amekufa juu ya Tawhiyd na si shirki. Inahusiana na mtu aliyekufa katika dhambi kubwa bila ya kuomba tawbah, kama mfano wa mwenye kufa katika uzinifu, kuomba, kula ribaa, kuwaasi wazazi, kukata udugu, kusengenya na kueneza uvumi na hakutubu. Huyu ndiye ambaye yuko chini ya matakwa ya Allaah. Kwa sharti asiwe ni mwenye kuhalalisha chochote katika mambo hayo ya haramu. Anajua kuwa uzinzi ni haramu, lakini matamanio yamemzidi. Anajua kuwa ribaa ni haramu, lakini hata hivyo akala ribaa kwa kupenda mali. Ama kuhusiana na mtu mwenye kuhalalisha ribaa, uzinzi au kuwaasi wazazi, huyu ni kafiri kwa sababu anamkadhibisha Allaah na Mtume Wake kwa kuharamisha mambo haya.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hidaayah ar-Rabbaaniyyah fiy Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (01/516)
  • Imechapishwa: 19/05/2020