Mke kuomba talaka kwa mume wake bila ya sababu yoyote


Swali: Je, inajuzu kwa mwanamke kuomba Talaka kwa mume wake na lini anaweza kuomba?

Jibu: Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwanamke yeyoye atakayeomba Talaka kutoka kwa mume wake bila ya sababu yoyote, ni kaharamishiwa harufu ya Pepo.”

Tunachomnasihi ni yeye kuwa na subira, na subira kwa mume wake na jamaa zake huzingatiwa ni katika aina bora ya ´amali anazojikurubisha nazo mja kwa Allaah. Kama jinsi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivyomuamrisha mume kuwa naye na subira na akasema:

“Mwanaume asimchukie muumini mwanamke, akichukia tabia fulani kutoka kwake atapenda nyingine alionayo.”

Masuala haya ni lazima pande zote mbili kuwa na subira, la sivyo mwanamke ambaye hana subira ataachika kila mwaka na kuolewa na mume mpya. Hali kadhalika, mume ambaye hana subira hali itakuwa ni hii hii. Allaah (´Azza wa Jalla) Anasema:

وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ

“Shirikianeni katika wema na taqwa, na wala msishirikiane katika dhambi na uadui.” (05:02)

Allaah (´Azza wa Jalla) Anasema:

الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّـهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَبِمَا أَنفَقُوا مِنْ أَمْوَالِهِمْ

“Wanaume ni wasimamizi juu ya wanawake kwa kuwa Allaah Amefadhilisha baadhi yao kuliko wengine na kwa sababu ya (matumizi) wanayotoa katika mali zao.” (04:34)

فَالصَّالِحَاتُ قَانِتَاتٌ حَافِظَاتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّـهُ ۚ وَاللَّاتِي تَخَافُونَ نُشُوزَهُنَّ فَعِظُوهُنَّ وَاهْجُرُوهُنَّ فِي الْمَضَاجِعِ وَاضْرِبُوهُنَّ ۖ فَإِنْ أَطَعْنَكُمْ فَلَا تَبْغُوا عَلَيْهِنَّ سَبِيلًا

“Basi wanawake wema watiifu, wenye kuhifadhi (hata) wanapokuwa hawapo (waume zao) kwa Aliyoyahifadhi Allaah. Na wale (wanawake) ambao mnakhofu uasi wao, basi waonyeni na (wakiendelea uasi) wahameni katika malazi (vitanda) na (mwishowe wakishikilia uasi) wapigeni. Wakikutiini, basi msitafute dhidi yao njia (ya kuwaudhi bure).” (04:34)

Hali kadhalika, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anasema: “Mwanamke ni mpungufu wa akili na Dini.”

Na anasema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kama ilivyokuja katika “Swahiyhayn”, Hadiyth ya Abu Hurayrah:

“Ninawausia kuwatendea wanawake wema, hakika wao wameumbwa kwa ubavu uliopinda… “

Tunachotaka kusema, ni lazima kuwa na subira kwa pande zote mbili sawa mume na mke. Na kuna ndugu zetu hapa ya kuwa kuna mwanaume aliyetalika wanawake watano katika siku moja. Alimtaliki wa kwanza. Akaja wa pili na kumuuliza: “Alikufanya nini?” Akamwambia: “Na wewe nimekutaliki.”

Akaja wa tatu na kumwambia: “Wewe ni mwanaume mwenye khasira, kwa nini umemtaliki?” Akamwambia: “Na wewe nimekutaliki.”

Akaja mke wa nne na kutaka kumpa nasaha. Akamwambia: “Na wewe nimekutaliki.” Na jirani wa nyumbani akamwambia: “Una nini wewe, wamekufanya nini?” Akamwambia: “Na wewe nimekutaliki mume wako akipitisha hilo.” Mume wake akasema: “Nimepitisha hilo.” Baada ya hilo ni lazima kuwa na subira kwa mwanaume na mwanamke. Sote ni wenye kughadhibika na tuna mapungufu mbalimbali. Ni lazima tuvumiliane na tumche Allaah.

  • Mhusika: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://muqbel.net/fatwa.php?fatwa_id=757
  • Imechapishwa: 27/02/2018