Mgonjwa wa pumu kutumia vidude vya oksijeni na vidonge vya unga


Swali: Kuna mtu ana ugonjwa wa pumu na hawezi kusoma Qur-aan mpaka atumie oksijeni. Je, aitumie mchana wa Ramadhaan?

Jibu: Ikiwa sio lazima kutumia vitu hivi vya oksijeni, basi bora asivitumie. Mfungaji si lazima kwake kusoma Qur-aan mpaka tuseme kuwa avitumie ili aweze kusoma Qur-aan. Hata hivyo wako watu wenye pumu ambao wanaogopa kukosa hewa pasi na vitu hivi vya oksijeni. Katika hali hiyo kutakuwa hakuna neno kutumia oksijeni hii. Kwa sababu kutokana na ninavojua hakuna chochote kinachofika tumboni; ni mishipa ya hewa tu ndio hufunguka. Mambo yakiwa hivo kweli basi hakuna neno. Lakini kuna aina nyingine ya vidonge wanavyopewa watu wenye pumu vya aina ya unga ambavo huyeyuka mdomoni na hivyo vikachanganyikana na mate. Vidonge hivi haijuzu kuvitumia wakati wa swawm ya lazima kwa sababu kile kinachochanganyikana na mate hatimaye hufika mpaka tumboni na hivyo vikamfunguza mfungaji. Ikiwa mtu mwenye pumu analazimika kuvitumia, basi swawm yake inaharibika na hivyo atatakiwa kuilipa siku hiyo. Na kama analazimika kuvitumia kila nyakati, basi atakula na kumlisha masikini kwa kila siku moja iliyompita.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (19/212-213)
  • Imechapishwa: 03/05/2021