Mgonjwa wa kifafa asiyeweza kufunga Ramadhaan

Swali: Mimi nimepatwa na maradhi ya kifafa na sikujaaliwa kufunga Ramadhaan kwa sababu nahitaji kumeza dawa mara tatu kwa siku. Nilijaribu kufunga siku mbili, lakini sikuweza. Aidha nimestaafu na pesa yangu ya staafu ni dinari 38 kwa mwezi. Nina mke na sina pato lingine zaidi ya pesa yangu ya staafu. Hukumu inasemaje ikiwa siwezi kulisha chakula mwezi huu?

Jibu: Ikiwa maradhi yanayokusumbua yanatarajiwa kupona basi unatakiwa kusubiri mpaka pale utakapopona kisha utalipa zile siku zilizokupita. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Basi atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu au yuko safarini, hivyo basi akamilishe idadi katika siku nyinginezo.”[1]

Ama ikiwa maradhi haya ni sugu yenye kuendelea, basi lililo la wajibu kwako ni kulisha masikini kwa kila siku moja iliyokupita. Inafaa vilevile kwako kutengeneza chakula cha mchana au cha jioni na ukawaalika masikini kwa kiasi cha yale masiku unayodaiwa na hivyo dhimma yako itakuwa yenye kutakasika kwa kufanya hivo. Sidhani kama kuna yeyote anayeshindwa kufanya hivo. Ikiwa huwezi kuwalisha masikini hawa wote katika mwezi mmoja, basi inafaa kuwagawanya kwa miezi mbalimbali kwa kiasi cha utakavoweza.

[1] 02:184-185

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (19/131-132)
  • Imechapishwa: 03/05/2021