Mfungaji kutumia dawa ya meno, matone ya machoni, masikioni na puani

Swali: Ni ipi hukumu ya kutumia dawa ya meno, matone ya masikioni, matone ya puani na dawa ya matone ya machoni kwa mfungaji? Mfungaji akihisi ladha yake afanye kitu gani?

Jibu: Kusafisha meno kwa dawa ya meno hakumfunguzi mfungaji kama mfano wa Siwaak. Muhimu ajitahidi kusiteremke kitu kooni mwake. Kikimshinda kitu katika hivyo pasi na kukusudia basi halazimiki kulipa. Vivyo hivyo matone ya machoni na ya masikioni hayamfunguzi mfungaji kutokana na maoni sahihi zaidi ya wanachuoni. Iwapo atahisi ladha ya matone kooni mwake basi kulipa kutakuwa ndio salama zaidi na wala sio wajibu. Kwa sababu huko hakuna maana ya kula wala kunywa.

Kuhusu kuweka dawa ya matone ya puani haijuzu. Kwa sababu puani kunaweza kupitishwa chakula. Kwa sababu hii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Fanya kishindo katika kupalizia isipokuwa kama utakuwa umefunga.”[1]

Aliyefanya hivo basi alipe kutokana na Hadiyth hii na zilizokuja kwa maana yake iwapo atahisi ladha kooni mwake.

[1] at-Tirmidhiy (788) na Abu Daawuud (142).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (15/260-261)
  • Imechapishwa: 26/05/2018