Swali: Ni ipi hukumu ya mtu ambaye ana ´Aqiydah ya Salaf na amesoma na kutakharuji kwa mfano katika kitivo cha Shari´ah, kitivo cha Da´wah au kitivo cha Hadiyth, anasema kuwa mfumo wa Salaf hauna maana yoyote katika Da´wah na kwamba badala yake anachagua mfumo wa al-Ikhwaan al-Muslimuun, Jamaa´at-ut-Tabliygh au mfumo mwingine. Aidha anasema kuwa hawadhuriki kitu kwa sababu ´Aqiydah yao ni ya Salaf lakini mfumo na Da´wah hausilihi. Je, Salaf walikuwa wakipambanua kati ya ´Aqiydah na mfumo katika Da´wah?

Jibu: Mfumo umejengeka katika ´Aqiydah. Yule ambaye ´Aqiydah yake ni salama basi hapana shaka kwamba mfumo wake pia utakuwa salama. Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipotaja yale mapote tatu na kwamba yote yataingia Motoni isipokuwa Moja tu, wakauliza ni kina nani hao [waliookoka]. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Ni wale wataokuwa juu ya yale niliyomo mimi hii leo na Maswahabah zangu.”

Bi maana katika ´Aqiydah, mfumo, matendo na kila kitu. Haiwezekani kimoja katika hivyo kikatofautiana na kingine.

Iwapo Ikhwaaniyyuun, Tabliyghiyyuun, Islaahiyyuun na wengineo watakuwa na mfumo usiopingana na Shari´ah, basi ni sawa. Na ikiwa unapingana na Shari´ah, basi ni lazima uwe umetokana na ´Aqiydah kwa sababu ni lazima kila kitendo kiwe kimejengeka juu ya nia. Ikiwa kila kitendo kimejengeka juu ya nia na mtu akachukua mfumo unaokwenda kinyume na mfumo wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na makhaliyfah zake waongofu, basi hiyo maana yake ni kwamba ´Aqiydah yake haikusalimika. Vinginevyo pale utaposalimika mfumo basi mfumo pia husalimika.

Kwa mnasaba huu napenda kusema kwamba mipasuko na migawanyiko ni balaa lililousibu Ummah na khaswa hii leo. Huyu ana mfumo fulani, mwengine ana mfumo fulani na kadhalika. Laiti basi wangeachana. Kila mmoja anamtia upotofuni mwingine. Pengine hata baadhi wakafikia kuwakufurisha wengine katika mambo ambayo sio upotofu wala sio ukafiri. Hili ni balaa lililoupata mwamsho wa kiislamu ambao tulikuwa na matumaini makubwa masiku ya nyuma. Leo vijana wengi wamefarikiana. Huenda mmoja katika vijana hawa akamchukia kijana mwengine anayetafuta haki zaidi kuliko anavomchukia mtu anayetenda madhambi makubwa. Yote haya ni katika ufunuo na fikira za shaytwaan. Ni lazima kwetu tuwe wakweli kati yetu na tuketi chini na kutafuta; tumnusuru ambaye anafuata haki na tumbainishie ambaye anafuata batili. Lakini ikiwa mtu atasema kuwa hataki jengine isipokuwa hilo na kwamba hiyo ni Ijtihaad yake yeye na kwamb anayo mashiko katika lugha ya kiarabu na katika dini, basi hatusemi kuwa ni mpotofu. Jambo ni lenye wasaa.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa’ al-Baab al-Maftuuh (128 B) Tarehe: 1417-02-04/1996-06-20
  • Imechapishwa: 15/07/2021