Mfano wa matendo mema katika masiku kumi ya mwanzo ya Dhul-Hijjah II

Matendo mema ni yenye kupendeza zaidi kwa Allaah katika masiku haya kumi ya mwanzo ya Dhul-Hijjah kuliko wakati mwingine wowote. Hebu wacha tuorodheshe baadhi ya matendo yaliyosuniwa khaswa katika masiku haya. Imesuniwa kumtaja Allaah. Allaah (Ta´ala) amesema:

لِّيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ عَلَىٰ مَا رَزَقَهُم مِّن بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ

”… ili wataje jina la Allaah kwa yale aliyowaruzuku ya wanyama hao.”[1]

Masiku yenye kujulikana ni haya masiku kumi ya Dhul-Hijjah. Kwa hivyo mtu anatakiwa kumtaja Allaah kwa wingi. Miongoni mwa Adhkaar ni kusema ”Allaahu Akbar”, ”Laa ilaaha illa Allaah” na ”Alhamdulillaah”. Aseme:

الله أكبر، الله أكبر، الله أكبر، لا إله إلا الله، والله أكبر، الله أكبر، ولله الحمد

”Allaah ni mkubwa, Allaah ni mkubwa, Allaah ni mkubwa, hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, Allaah ni mkubwa, Allaah ni mkubwa na himdi zote ni stahiki ya Allaah.”

Mtu anatakiwa kusema hivi kwa wingi. Mtu aseme hivo misikitini kwa sauti ya juu, masoko na majumbani.

Miongomi mwa matendo mema ni kufunga masiku haya kumi tukiondoa ile siku ya ´iyd. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiyafunga. Hayo yamepokelewa na Imaam Ahmad na watunzi wa Sunan kwamba Hafswah bint ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anhum) ya kwamba Mtume  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa haachi kuyafunga. Haya ndio maoni yenye nguvu.

Kuhusu Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) iliopokelewa na Muslim ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa hafundi katika masiku haya kumi, wanachuoni wamesema kwamba pindi watu waadilifu na waaminifu wawili wanapotofautiana ambapo mmoja ni mwenye kuthibitisha na mwingine anakanusha, basi anatanguliza yule mwenye kuthibitisha. Kwa sababu huyu wa pili ndiye mwenye ziada ya elimu. Ukanusha wa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) unaweza kutokana na kujua na si kukanusha utokeaji. Hivi ndivo tunavyooanisha kati ya Hadiyth hizi mbili.

Tukadirie kuwa Hadiyth ya Hafswah haikusihi, kufunga ni miongoni mwa matendo bora kabisa. Hivyo yanaingia ndani ya maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakuna masiku ambayo matendo mema yanapendwa zaidi na Allaah ndani yake kama  masiku haya kumi.”

Miongoni mwa mambo yaliyopendezwa katika masiku haya ni kusafiri kwenda katika Nyumba Tukufu ya Allaah kufanya ´Umrah na Hajj. Hiki ndio kitendo bora kabisa kinachoweza khaswa kufanywa katika masiku haya. Kwa msemo mwingine matendo mema katika masiku haya ambacho ni bora zaidi ni kusafiri kwenda katika Nyumba ya Allaah kutekeleza ´Umrah na Hajj. Hajj ni aina fulani ya jihaad katika njia ya Allaah.

Miongoni mwa mambo yanayofanywa ile siku ya mwisho ya masiku haya kumi ni kujikurubisha kwa Allaah kwa kuchinja. Kitendo hichi kinafanywa na yule ambaye hakuhiji. Kinafanywa na waislamu katika miji yao. Kuhusu mahujaji kilichosuniwa kwao ni Hady. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alichinja mnyama katika hijah yake na hakuchinja Udhhiyah ambapo akamchinja Madiynah katika mwaka ambao haukuwa wa Hajj.

[1] 22:34

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binothaimeen.net/content/17549
  • Imechapishwa: 25/07/2020