Mazingatio makubwa kwa mlinganizi na yule mwenye kulinganiwa

397- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna Mtume katika Mitume aliyesadikishwa kama nilivosadikishwa. Wako katika Mitume ambao hawakuaminiwa na watu katika Ummah zao isipokuwa mtu mmoja tu.”

Ameipokea Ibn Hibbaan[1]. Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh na imepokelewa na Muslim[2].

Katika Hadiyth kuna dalili ya wazi kabisa inayoonyesha kuwa wingi au uchache wa wafuasi sio kipambanuzi chenye kuonyesha kuwa mlinganizi yuko katika haki au batili. Pamoja na kuwa Mitume hawa (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) Da´wah na dini yao ilikuwa moja idadi ya wafuasi wao ilikuwa ni yenye kutofautiana. Hali ilikuwa inaweza kufikia kiasi cha kwamba baadhi yao wanasafikishwa na mfuasi mmoja tu na wengine hawasadikishwi na mtu hata mmoja.

Hapa kuna mazingatio makubwa kwa mlinganizi na yule anayelinganiwa katika zama hizi. Mlinganizi anatakiwa kutafakari uhakika huu. Ni lazima kwake kupambana katika njia ya Allaah (Ta´ala) na wala asijali uchache wa wale wenye kumuitikia. Kwa sababu yeye hana kazi nyingine isipokuwa kufikisha kwa njia iliokuwa wazi na yeye ana kiigizo chema kwa wale Mitume waliotangulia ambao walikuwa na mfuasi mmoja au wawili tu.

Wale wanaolinganiwa hawatakiwi kuhisi vibaya kutokana na ule uchache wa watu wanaomuitikia yule mlinganizi. Kitendo cha watu wachache kuitikia wito wa mlinganizi hakitakiwi kuwafanya wakatilia mashaka juu ya Da´wah ya kweli na wakaacha kuiamini, seuze wasichukulie kitendo hicho kuwa ndio dalili yenye kuonyesha kuwa Da´wah yake ni ya batili kwa sababu tu eti hakuna yeyote aliyemfuata. Mtu kusikilizwa na watu wengi haina manaa kwamba Da´wah yake ni ya haki. Kwani Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَمَا أَكْثَرُ النَّاسِ وَلَوْ حَرَصْتَ بِمُؤْمِنِينَ

“Wengi wa watu hawatoamini ijapokuwa utalitilia hima.”[3]

[1] 2305.

[2] 1/130.

[3] 12:103

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah (1/2/755-756)
  • Imechapishwa: 17/05/2019