Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ أَبَىٰ وَاسْتَكْبَرَ وَكَانَ مِنَ الْكَافِرِينَ

”Kumbuka Tulipowaambia Malaika: ”Msujudieni Aadam”, wakasujudu isipokuwa Ibliys alikataa na akatakabari na akawa miongoni mwa makafiri.”[1]

Kisha tukawaamrisha kumsujudia Aadam kwa sababu ya kumuheshimisha na kumtukuza na kumwabudu Allaah (Ta´ala). Wakatekeleza amri ya Allaah na wakaharakisha wote kusujudu isipokuwa tu Ibliys ambaye alikataa kusujudu na akafanya kiburi juu ya amri ya Allaah na juu ya Aadam. Alisema:

أَأَسْجُدُ لِمَنْ خَلَقْتَ طِينًا

“Je, nimsujudie Yule uliyemuumba kwa udongo?”[2]

Kukataa huku na kiburi ni natija ya ukafiri alionao. Hapo ndipo kulipobaini uadui wake kwa Allaah na kwa Aadam na ukafiri na kiburi chake.

Katika Aayah hii kuna mazingatio na alama:

1 – Kuna uthibitisho wa maneno ya Allaah na kwamba bado ni Mwenye kuendelea kuzungumza. Anasema akitakacho, anatamka akitakacho na kwamba Yeye ni mjuzi wa yote na Mwenye hekima.

2 – Mja asipojua hekima ya Allaah juu ya baadhi ya viumbe au maamrisho, basi lililo wajibu kwake ni kujisalimisha, kuituhumu akili yake na kumthibitishia Allaah hekima.

3 – Allaah kuwajali Malaika na kuwafanyia wema kwa kuwafunza yale wasiyoyajua na kuwazindua yale wasiyoyajua.

4 – Ndani yake pia kuna fadhilah za elimu kwa njia nyingi ikiwa ni pamoja na:

1 – Allaah amewajuza Malaika kwa elimu na hekima Yake.

2 – Allaah amewatambulisha ubora wa Aadam kwa elimu na kwamba ndio sifa bora anayoweza kuwa nayo mja.

3 – Allaah amewaamrisha kumsujudia Aadam kwa sababu ya kumuheshimisha ilipobainisha ubora wa elimu.

4 – Mtihani kwa mwengine akishindwa kwa kile alichopewa mtihani kwacho kisha akakitambua yule mwenye fadhilah, basi yeye ni mkamilifu zaidi kuliko aliyeanza kukitambua.

5 – Mazingatio juu ya baba wa majini na watu na ubainifu wa ubora wa Aadam, namna Allaah alivyomfadhilisha na Ibliys akamfanyia uadui.

Yapo mazingatio mengine pia.

[1] 02:34

[2] 17:61

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-Kariym, uk. 39
  • Imechapishwa: 15/06/2020