Mavazi ya Salaf katika zile siku kumi za mwisho za Ramadhaan

Ibn Jariyr amesema:

“Walikuwa wakipendelea kuoga katika kila usiku miongoni mwa zile nyusiku kumi za mwisho.”

 an-Nakha´iy alikuwa akioga kila usiku katika zile nyusiku kumi za mwisho. Wako ambao walikuwa wakioga na wakijitia manukato katika zile nyusiku ambazo kuna matarajio na dhana yenye nguvu kwamba ni usiku wa Qadr. Kwa mfano Zirr bi Hubaysh ameamrisha kuoga usiku wa tarehe ishirini na saba. Imepokelewa kwamba ilipokuwa inafika usiku wa tarehe ishirini na nne basi Anas bin Malik (Radhiya Allaahu ´anh) alikuwa akioga, akijitia manukato na akivaa nguo zake nzuri kabisa. Unapokwisha usiku huo, basi anazikunja na hazitumii tena mpaka tarehe ishirini na nne mwaka unaofuata.

Ayyuub as-Sikhtiyaaniy alikuwa akioga usiku wa tarehe ishirini na tatu na usiku wa tarehe ishirini na nne. Huvaa nguo nzuri na akijifukiza. Alikuwa akisema:

“Usiku wa tarehe ishirini na tatu ndio usiku wa watu wa Madiynah na usiku wa tarehe ishirini na nne ndio usiku wetu.”

Bi maana watu wa Baswrah.

Thaabit al-Bunaaniy na Humayd at-Twawiyl walikuwa wakivaa nguo zao nzuri kabisa na wakijitia manukato. Walikuwa wakiutia msikiti manukato na wakiufukiza katika ule usiku ambao kuna matarajio makubwa kwamba ndio usiku wa Qadr. Thaabit amesema:

“Tamiym ad-Daariy alikuwa na shuka ya juu ambayo aliinunua dirhamu elfu. Shuka hii ya juu alikuwa akiivaa katika usiku ambao kuna matarajio makubwa kwamba ndio usiku wa Qadr.”

Haya yanajulisha kwamba imependekezwa katika ule usiku ambao kuna matarajio kuwa ndio usiku wa Qadr watu wajisafishe, waoge, wajipambe, wajitie manukato na wavae mavazi yaliyo mazuri kama ambavo imesuniwa kufanya hivo katika swalah za ijumaa na swalah za ´iyd. Vivyo hivyo ni jambo limewekwa katika Shari´ah kujipamba katika swalah zengine zote. Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا بَنِي آدَمَ خُذُوا زِينَتَكُمْ عِندَ كُلِّ مَسْجِدٍ

“Enyi wana wa Aadam! Chukueni mapambo yenu katika kila swalah.”[1]

Ibn ´Umar amesema:

“Allaah ana haki zaidi ya kupambiwa.”

Lakini kujipamba kwa uinje hakutimii mpaka kwanza mtu ajipambe kwa ndani. Mapambo ya ndani ni kule mtu kutubia na kurejea kwa Allaah na kujisafisha kutokamana na uchafu wa madhambi. Kwani mapambo ya nje pamoja na kuharibika kwa ndani si lolote si chochote. Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا بَنِي آدَمَ قَدْ أَنزَلْنَا عَلَيْكُمْ لِبَاسًا يُوَارِي سَوْآتِكُمْ وَرِيشًا ۖ وَلِبَاسُ التَّقْوَىٰ ذَٰلِكَ خَيْرٌ

“Enyi wana wa Aadam! Hakika Tumekuteremshieni mavazi yanayoficha sehemu zenu za siri na nguo za pambo; na vazi la kumcha Allaah ndiyo bora zaidi.”[2]

[1] 07:31

[2] 07:26

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Latwaa’if-ul-Ma´aarif, uk. 260
  • Imechapishwa: 14/05/2020