Maulidi sio katika Shari´ah ya Allaah


Swali: Ni ipi hukumu ya kusherehekea siku ya kuzaliwa?

Jibu: Kusherehekea siku ya kuzaliwa ni jambo lisilokuwa na msingi katika Shari´ah. Bali ni katika Bid´ah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayezua katika amri yetu hii yale yasiyokuwemo atarudishiwa mwenyewe.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Katika upokezi wa Muslim imekuja:

“Atakayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu atarudishiwa mwenyewe.”

Ni jambo linalojulikana ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakupatapo kusherehekea mazazi yake kwa kipindi cha maisha yake na wala hakuamrisha yafanywe. Vilevile hayakufanywa na Maswahabah wala wale makhaliyfah waongofu. Bali Maswahabah wake wote hawakuyafanya ilihali wao ndio watu wajuzi zaidi wa Sunnah zake na ndio wanaompenda zaidi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wenye pupa zaidi ya kufuata yale aliyokuja nayo. Lau kusherehekea mazazi yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ingelikuwa ni kheri basi wangeliyakimbilia. Vivyo hivyo wanachuoni katika zile karne bora hawakuyafanya na wala hawakuyaamrisha.

Hivyo ikapata kujulikana ya kwamba sio katika Shari´ah ambayo Allaah amemtuma kwayo Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Sisi tunamshuhudisha Allaah na waislamu wote ya kwamba endapo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angeliyafanya au Maswahabah wake (Radhiya Allaahu ´anhum) basi na sisi kadhalika tungeliyafanya, tukayaamrisha, tukayakimbilia na kulingania kwayo. Kwa sababu sisi – na himdi zote zinarejea kwa Allaah – ni miongoni mwa watu wenye pupa zaidi juu ya kufuata Sunnah zake, kuadhimisha maamrisho na makatazo yake.

Tunamuomba Allaah sisi na waislamu wote atuthibitishe katika haki na atulisalimishe kutokamana na yale yote yanayopingana na Shari´ah Yake safi. Kwani hakika Yeye ni Mwingi wa kutoa, mkarimu.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (04/285)
  • Imechapishwa: 29/07/2017