Matendo yanaweza kuwa sababu ya kumtoa mtu nje ya Uislamu

Swali: Yapi maoni yako kwa mwenye kusema ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kanuni ya kuwa muislamu hakufuru kwa dhambi mpaka ahalalishe ni kama ilivyo, na kwamba hakuna dhambi anayokufuru nayo mtu na kumtoa katika Uislamu hata ikiwa kwa mfano ni kusujudia kaburi au kulifanyia Twawaaf au kuifanyia maskhara dini ya Uislamu n.k?

Jibu: Sababu za mtu kukufuru ni nyingi. Miongoni mwazo ni mtu kuitakidi kujuzu kusujudu kwa asiyekuwa Allaah hata kama yeye hakusujudu. Anakuwa kafiri.

Na miongoni mwazo afanyie maskhara Uislamu hata kama atakuwa ni mwenye kufanya mzaha tu. Ni kafiri. Dalili:

قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Sema:  Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake?”  Msitoe udhuru; mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.” (09:65-66)

Kuna matendo ambayo ni kufuru. Mwenye kuyafanya anahesabika kuwa ni kafiri na anaamiliwa duniani matangamano ya kafiri. Na Aakhirah hesabu yake iko kwa Allaah.

Kwa mfano tunaona mtu kasujudia sanamu tunamhukumu ukafiri, na tunasema kuwa ni kafiri. Ataombwa kutubia la sivyo anauawa sawa ikiwa atasujudu kwa unyenyekevu, akawa amekusudia kulisalimia. Sisi hatujali hili. Mtume (swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kasema:

“Lau ningelimwamrisha mtu kumsujudia mwengine, basi ningemwamrisha mwanamke kumsujudia mume wake.”

Katika matendo ambayo ni kufuru, ni mtu kuacha swalah. Swalah mwenye kuiacha tunamhukumu kwa ukafiri binafsi. Wala hatusemi kiujumla mwenye kuacha swalah ni kafiri. Tunasema hivyo pia, lakini tunapomuona mtu haswali tunamhukumu ukafiri na kuhalalisha damu yake. Isipokuwa ikiwa atatubu na kurejea kwa Allaah.

Muhimu ni kuwa kanuni ulioitaja haifahamiki hivyo moja kwa moja. Kwa kuwa tungelisema hakuna kufuru isipokuwa mpaka mtu ahalalishe tu, pasingelikuwepo kufuru ya matendo moja kwa moja. Kwa kuwa kule kuhalalisha kwenyewe tu ni ukafiri. Mtu akihalalisha kitu ambacho wamekubaliana wanachuoni wote uharamu wake, ni kafiri. Sawa ikiwa yeye atakifanya au kutokifanya. Kwa mfano mtu akahalalisha Zinaa, Ribaa katika mambo ambayo hakuna tofauti, tungelisema huyu ni kafiri.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa’ al-Baab al-Maftuuh (163 B) Tarehe: 1418-03-20/1997-07-25
  • Imechapishwa: 10/04/2022