Matanga yote ni Bid´ah


Swali: Ni ipi hukumu ya matanga?

Jibu: Matanga yote ni Bid´ah hata kama ni siku tatu, wiki au siku arubaini. Ni jambo halikuthibiti kutoka katika matendo ya wema waliotangulia (Radhiya Allaahu ´anhum). Ingelikuwa kheri basi wangelitutangulia kulifanya. Jengine ni kwamba ni kupoteza mali, wakati na huenda kukatokea ndani yake maovu kama kujipiga na maombolezo, mambo ambayo yanaingia katika laana. Hakika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemlaani muombolezaji na yule msikilizaji.

Halafu isitoshe ikiwa ni katika mali ya maiti – namaanisha ile thuluthi yake – itakuwa ni kumfanyia vibaya. Kwa kuwa ni kuitoa katika maasi. Ikiwa ni katika mali ya warithi, ikiwa katika wao kuna wadogo na wajinga wasioweza kuendesha mambo, itakuwa vilevile ni kuwafanyia vibaya. Kwa sababu mtu ni mwenye kupewa amani katika mali yake na haifai kuitumia isipokuwa katika yenye kumnufaisha. Wakiwa ni wenye busara, wamekwishabaleghe na kupevuka ni upumbavu vilevile. Kutumia mali katika mambo yasiyomkurubisha mtu mbele ya Allaah au kwenye mambo ambayo mtu hanufaiki nayo duniani ni miongoni mwa mambo yanayohesabika kuwa ni upumbavu. Utumiaji pesa huo utazingatiwa kuwa ni kupoteza mali. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kupoteza mali.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (02/305)
  • Imechapishwa: 04/06/2017