Swali: Umezungumzia kuhusu Qunuut wakati wa majanga. Naomba utubainishie yafuatayo kwa sababu ni mambo yametutatiza. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiomba dhidi ya Ra´aliy, Dhukwaan na ´Uswayyah. Kwa hivyo tunaomba utuwee wazi jambo hili; je, mtu anasoma ndani yake du´aa isemayo:

اللهم اهدنا فيمن هديت

“Ee Allaah! Niongoze pamoja na wale Uliowaongoza… “

Je, inafaa kurefusha na mtu akatoka nje ya maudhui ambayo ni kuwatakia nusura wale waliofikwa na majanga? Je, wanaombewa waislamu wote kwa ujumla, mtu anaomba dhidi ya makafiri na mtu anasema:

ربنا آتنا في الدنيا حسنة

“Ee Allaah! Tupe mazuri ya dunia… “

pamoja na kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?

Jibu: Kwanza tunatakiwa kujua kuwa Qunuut wakati wa majanga amri yake imeegemezwa kwa mtawala na mfalme. Mpaka Fuqahaa´ wa Hanaabilah (Rahimahumu Allaah) wanaona kwamba haifai kukunuti isipokuwa kiongozi peke yake. Hatukusudii imamu wa msikiti. Tunakusudia kiongozi wa nchi peke yake. Ikiwa ni jambo limeegemezwa kwa kiongozi basi haifai kwa mtu kukunuti pasi na idhini yake. Hili ni mosi. Haya ni masuala muhimu sana.

Jambo la pili mtu afanye Qunuut katika swalah ya Fajr peke yake au katika swalah zote? Jibu ni kwamba inakuwa katika swalah zote. Hivo ndivo ilivyothibiti kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini mtawala akisema watu wakunuti katika swalah ya Fajr, hiyo maana yake kwamba tusikunuti katika swalah nyenginezo.

Jambo la tatu Qunuut ni ile du´aa inayotambulika inayosomwa katika Witr “Ee Allaah niongoze pamoja na wale Uliowaongoza”? Hapana. Mambo sivyo. Qunuut inakuwa kwa yale yanayohusiana peke yake. Kwa mfano ikiwa hivi sasa tunakunuti kwa ajili ya ndugu zetu wa Kosovo, basi tunawaombea Allaah (Ta´ala) awanusuru dhidi ya maadui wao na awatokomeze maadui wao. Huu ndio msingi. Mtu akizidisha juu yake kwa kumshukuru Allaah (´Azza wa Jall), kumsifu, kumswalia Mtume Wake na kuwaombea du´aa waislamu ni sawa. Lakini asirefushe. Kwani baadhi ya watu wanarefusha katika Qunuut mpaka wanachoka waswaliji nyuma yake. Hili ni kosa. Tukijua kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye ndiye kiigizo na ruwaza yetu njema, harefushi katika Qunuut ya majanga, basi tumuige yeye.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (63) http://binothaimeen.net/content/1448
  • Imechapishwa: 30/12/2019