Masharti ya Ruqyah ya kishari´ah


Kwa hiyo, Ruqyah yenye kunufaisha ni ile ambayo imeeneza masharti haya.

1) Ruqyah iwe inatokana na Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Na dawa zinazoruhusiwa, au dawa zinazoafikiana na zile zilizowekwa. Kusiwe ndani yake na dawa za ki-Shirki au dawa za ki-Bid´ah, isipokuwa iwe ni dawa zenye kunufaisha, zilizotakasika na Shirki. Na hili hakuna anayelijua isipokuwa ni wanachuoni. Ikiwa mtu ana uwezo wa kujua Ruqyah hii ya Kishari´ah, Alhamdulillaah. La sivyo, awaulize Ahl-ul-´Ilm na Ahl-ul-Baswiyrah. Na asimuulize mtu ni mtu tu miongoni mwa watu wenye haraka, wajinga na wapotevu. Badala yake awaulize wanachuoni, waaminifu na wenye kumuamini Allaah (´Azza wa Jalla). Hii ndio sharti ya kwanza.

2) Msomaji awe ni katika watu wa Tawhiyd, wanachuoni na watu wenye ´Aqiydah iliyo salama. Asiende kwa waganga, Mashaytwaan na wachawi akaomba Ruqyah kutoka kwao, hata kama watu wanawataja watu hawa na kuwaelekeza watu kwao, asiwaendee. Anasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atakayemwendea kuhani, hazitokubaliwa Swalah zake kwa siku arubaini.”

Na katika Hadiyth nyingine: “Atakayemwendea kuhani au mpiga ramli na akamsadikisha kwa alichokisema, kakufuru kwa aliyoteremshiwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Watu hawa ni makuhani, wachawi na Mashaytwaan. Au pengine ni wajinga wasiojua haki kutokana na batili, wao wanachotaka ni mali tu na wala hawaulizi kuwa ni haki wala batili. Wasiendewe watu hawa. Na yasemekana kuwa, miongoni mwao wanawaamrisha wanaowaendea kuchinja kwa ajili ya asiyekuwa Allaah, kisha ndio wanawafanyia mahitajio yao. Na hii ni Shirki kubwa inayomtoa mtu katika Uislamu. Usiwaendee watu wasiojulikana au wanaojulikana kwa shari, au wanaojulikana kwa Shirki na uchawi.

3) Ruqyah anayoisoma msomaji iwe kwa maneno ya kiarabu yanayofahamika. Ruqyah isiwe kwa matamshi ya kigeni au matamshi yasiyotambulika maana yake. Pengine ikawa ni majina ya Mashaytwaan na majini, anawaomba huyu mchawi badala ya Allaah (´Azza wa Jalla). Na msomewaji hafahamu lugha yake na wala hajui akisemacho. Watu hawa husema maneno wasiyoyafahamu waliohudhuria pale wala mgonjwa. Huyu haijuzu kwenda kwake. Kwa kuwa maneno haya yasiyofahamika maana yake yanaweza kuwa ni kutafuta kinga kwa Shaytwaan au ni maombi kwa asiyekuwa Allaah (´Azza wa Jalla). Akawa mtu huyu ni katika Mashaytwaan, makuhani, wachawi na waganga.

4) Mtu aitakidi kuwa mponyeshaji ni Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Na Ruqyah ya Kishari´ah ni sababu tu. Akipenda Allaah itamfaa na kama Hakupenda Haitomfaa kitu. Mambo yako Mikononi mwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Asiitakidi Ruqyah kuwa ndio inaponyesha maradhi, lakini kinyume chake amuamini Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na kuchukulia kuwa Ruqyah hii ni sababu miongoni mwa sababu Alizoweka Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Yakitimia masharti haya, hii itakuwa ni Ruqyah ya Kishari´ah, yenye kuaminika na yenye kunufaisha kwa idhini ya Allaah (´Azza wa Jalla).

Lakini baadhi ya watu hawakinaiki na Ruqyah hii ya Kishari´ah, badala yake wanawaendea Mashaytwaan hawa na wachawi na kusema kuwa “watu hawa walitibiwa kwa fulani n.k.”. Hawakinaiki na Ruqyah ya Kishari´ah. Wanaiuza Dini yao – A´udhubi Allaah – na kuzivunja ´Aqiydah zao kwa na wanatoka katika maradhi madogo na kwenda katika maradhi makubwa, nayo ni maradhi ya Shirki na kuiharibu ´Aqiydah.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaa
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://www.youtube.com/watch?v=yju6BpZSJ7g
  • Imechapishwa: 20/03/2018