Swali: Mimi ni mshairi. Kuna mtu rafiki yangu kipenzi wa karibu alifariki. Katika maombolezo yangu nikamtungia misitari ya mashairi. Kisha nikaenda makaburini kusomea nayo kama anavyofanya yule anayetaka kumtolea salamu. Je, kitendo changu hichi ni sahihi? Je, maiti huyu anasikia maombolezo yake?

Jibu: Lau usingelifanya haya na badala yake ukampa ile karatasi akajisomea mwenyewe ingelikuwa bora. Hili ni jambo halikuwekwa katika Shari´ah na ni kosa ulifanya. Maiti haisikii mfano wa haya. Kikubwa anachoweza kusikia ni kwamba mwenye kumtolea salamu ilihali anamjua basi anamuitikia. Hapa ni pale ambapo Hadiyth iliopokelewa juu ya hilo itakuwa ni Swahiyh. Kwa sababu wanachuoni wametofautiana juu ya kusihi kwa Hadiyth hiyo:

“Mtu anapoliendea kaburi la mtu ambaye alikuwa anamfahamu duniani na akamtolea salamu, basi Allaah anamrudishia roho yake ambapo anamuitikia salamu.”

Hapa ni pale ambapo Hadiyth itakuwa imesihi. Ama kuomboleza kwa kumtungia mashairi na kuanza kumuimbia, si sahihi. Hapana shaka kwamba ni Bid´ah.

Mimi nawanasihi ndugu zangu wasizichoshe nafsi zao kufungamana na wafu. Wakifungamana na wafu na wakakithirisha kuwatembelea ndugu na marafiki, basi huzuni itakuwa mioyoni mwao na haitoondoka. Itakuwa kila wanapowatembelea basi wanapata huzuni upya. Kila aliyehai atakufa. Msiba unasahaulika kadiri na siku zinavyokwenda ikiwa hakupatikana yale mambo yanayoufanya kuwa mpya. Inatosha kumtendea wema maiti – sawa awe ni ndugu au rafiki – kumuombea du´aa kwa Allaah. Hii ndio zawadi bora unayoweza kumpa maiti. Muombee du´aa kwa Allaah, muombee msamaha na du´aa aina mbalimbali nzuri.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (60) http://binothaimeen.net/content/1368
  • Imechapishwa: 27/11/2019