Maradhi aina mbili katika Ramadhaan

Swali: Mgonjwa ambaye analazimika kulisha chakula inafaa kwake kuwapa chakula hicho wasiokuwa waislamu ikiwa ni katika nchi za makafiri?

Jibu: Kwanza tunapasa kutambua kuwa maradhi yamegawanyika aina mbili:

1 – Maradhi yanayotarajiwa kupona kama yale yanayozuka ghafla. Haya Allaah (Ta´ala) anasema:

فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Basi atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu au yuko safarini, hivyo basi akamilishe idadi katika siku nyinginezo.”[1]

Katika hali hii mgonjwa huyu anatakiwa kusubiri mpaka pale atakapopona kisha atalipa. Ikiwa atakufa kabla ya kupona, basi hakuna kinachomlazimu. Kwa sababu Allaah amemuwajibikia kulipa katika masiku mengine, amekufa kabla ya kukutana na masiku hayo. Ni kama ambaye amekufa katika Sha´baan kabla ya kuingia Ramadhaan; hakuna anayewajibika kufunga kwa niaba yake.

2 – Maradhi sugu na yasiyotarajiwa kupona kama vile saratani, figo na kisukari – Allaah atulinde kutokamana nayo. Katika hali hii mgonjwa huyu anatakiwa kuacha kufunga na badala yake alishe masikini kwa kila siku moja aliyoacha kufunga. Ni kama mfano wa mtumzima kikongwe asiyeweza kufunga; anatakiwa kuacha kufunga na badala yake atoe chakula kumlisha masikini kwa kila siku moja iliyompita. Dalili ya hilo ndani ya Qur-aan ni maneno Yake Allaah (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ  أَيَّامًا مَّعْدُودَاتٍ ۚ فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۚ وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ

”Enyi walioamini! Mmefaridhishwa kufunga kama ilivyofaridhishwa kwa walio kabla yenu mpate kumcha. Ni siku za kuhesabika. Lakini atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu au yuko safarini, basi [akamilishe] idadi katika siku nyenginezo. Na kwa wale wanaoiweza lakini kwa tabu basi watoe fidia: kulisha masikini.”[2]

Hapo mwanzoni ilikuwa wale wenye kuweza kufunga lakini hawataki basi wanatakiwa kuwalisha masikini licha ya kuwa kufunga ndio ilikuwa bora. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَأَن تَصُومُوا خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ

”Mkifunga ni bora kwenu mkiwa mnajua.”[3]

Kipindi hicho mtu alikuwa na khiyari ya ima kufunga au kulisha chakula. Baadaye ikawa kufunga ni lazima kwa kila mmoja:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ  أَيَّامًا مَّعْدُودَاتٍ ۚ فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۚ وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ

”Enyi walioamini! Mmefaridhishwa kufunga kama ilivyofaridhishwa kwa walio kabla yenu mpate kumcha. Ni siku za kuhesabika. Lakini atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu au yuko safarini, basi [akamilishe] idadi katika siku nyenginezo. Na kwa wale wanaoiweza lakini kwa tabu basi watoe fidia: kulisha masikini.”

Kukafanywa kufunga badala ya kutoa chakula. Ambaye hawezi kufunga kabisa, si wakati wa Ramadhaan wala wakati mwingine, basi anatakiwa kutoa chakula. Yule mwenye maradhi sugu na mzee kikongwe asiyeweza kufunga, pasi na kujali ni mume au mke, basi anatakiwa kulisha masikini kwa kila siku moja. Ima anaweza kuwagawanyia chakula au pia anaweza kuwaalika katika chakula. Hilo la pili lilikuwa likifanywa na Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) baada ya kuwa mtumzima kikongwe; alikuwa akialika masikini thelathini katika chakula cha jioni.

Kwa kumalizia ni kwamba maradhi yamegawanyika aina mbili: maradhi yaliyozuka yanayotarajiwa kupona na maradhi sugu yasiyotarajiwa kupona: maradhi yaliyozuka na yanayotarajiwa kupona anapaswa kusubiri mpaka pale Allaah atakapomponya kisha atalipa. Yule mwenye maradhi sugu yasiyotarajiwa kupona anatakiwa kumlisha masikini chakula kwa kila siku moja iiyompita.

Ama ikiwa mtu anaishi katika nchi isiyokuwa ya Kiislamu na anawajibika kutoa chakula, basi anatakiwa kuwapa chakula. Vinginevyo atatakiwa kuiagiza katika nchi yoyote ya Kiislamu ambayo watu wake wanahitajia chakula hichi.

[1] 02:184-185

[2] 2:183-184

[3] 02:184

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (19/111-112)
  • Imechapishwa: 11/05/2021