Maoni ya Shaykh-ul-Islaam na Ibn ´Uthaymiyn juu ya ni lini msafiri anatakiwa kufupisha swalah

Swali: Sisi ni vijana ambao tulitoka katika safari ya ardhini baada ya swalah ya Fajr mpaka saa nne usiku. Sehemu hiyo ilikuwa mbali na mji wetu kwa kilomita 170. Wakati tulipowajibikiwa na swalah ya ´Aswr tuliswali Dhuhr na ´Aswr kwa kukusanya na kufupisha. Kuna mmoja wetu alikusanya na hakufupisha. Ni ipi hukumu ya swalah zao pamoja na kuwa hawakusafiri?

Jibu: Masuala haya yana tofauti kwa wanachuoni. Kuna katika wanachuoni walioweka mpaka wa umbali maalum. Kuna wengine walifanya kwamba jambo hilo linategemea na desturi za watu. Wale walioweka mpaka maalum walisema inapozidi 83 km basi mtu anazingatiwa kuwa ni msafiri. Katika hali hii anatakiwa kufupisha na kukusanya pale anapohitajia kufanya hivo. Kukusanya sio katika rukhusa za  safari katika hali zote. Bali lililo bora kwa msafiri ambaye ametua mahali aache kufanya hivo tofauti na yule ambaye bado yunjiani. Kuhusu kufupisha imependekezwa kwa msafiri japokuwa atakuwa ametua pahala.

Wako wanachuoni wengine wenye kuoenela kuwa safari haikuwekewa kikomo cha umbali maalum. Safari ni ile ambayo watu wameizingatia kuwa ni safari na wamezowea hivo. Hili la pili ndio chaguo la Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah. Kujengea juu ya hili tunasema mtu akitoka katika mji wake karibu 70 km, 80 km, 100 km au zaidi ya hapo na mwishoni mwa mchana mtu anaweza kurudi kwa ukaribu – kwa njia ya kwamba mtu anaweza kutoka asubuhi na akarudi mwishoni mwa mchana – hii haizingatiwi safari kwa watu. Lililo salama zaidi kwake aswali Rakaa´ nne na aswali kila swalah kwa wakati wake.

Mimi naona kuwa watu hawa wanatakiwa kuswali pasi na kufupisha. Vilevile wasikusanye. Isipokuwa haja ikipelekea kukusanya basi wafanye hivo pasi na kufupisha.

Mimi napenda kutoka kwa ndugu wasitofautiane. Kwa mfano watu hawa wametofautiani kwa njia ya kwamba kuna wenye kuonelea kufupisha na wengine hawaonelei hivo, wamoja wanaonelea kukusanya na wengine hawaonelei hivo, tunaweza kuwafanya wamoja wote na tukawaambia waswali kikamilifu na waswali kila kila kwa wakati wake na hatimaye mkazitekeleza bila tofauti.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (38) http://binothaimeen.net/content/877
  • Imechapishwa: 10/08/2018