Maoni sahihi ni kwamba Khul´ haizingatiwi ni talaka

Maoni yenye nguvu ni kwamba Khul´ (mwanamke kujivua katika ndoa) sio talaka ijapokuwa itatokea waziwazi kwa tamko la talaka. Dalili ya hilo ni Qur-aan tukufu. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

الطَّلَاقُ مَرَّتَانِ ۖ فَإِمْسَاكٌ بِمَعْرُوفٍ أَوْ تَسْرِيحٌ بِإِحْسَانٍ

“Talaka ni mara mbili. Hivyo kuzuia kwa mujibu wa Shari´ah au kuachia kwa wema.”

Bi maana katika hiyo mara ya pili. Ima mtu abaki naye au amwachie kwa wema. Jambo liko mikononi mwako mwanamme:

وَلَا يَحِلُّ لَكُمْ أَن تَأْخُذُوا مِمَّا آتَيْتُمُوهُنَّ شَيْئًا إِلَّا أَن يَخَافَا أَلَّا يُقِيمَا حُدُودَ اللَّـهِ ۖ فَإِنْ خِفْتُمْ أَلَّا يُقِيمَا حُدُودَ اللَّـهِ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِمَا فِيمَا افْتَدَتْ بِهِ

”Wala si halali kwenu kuchukua chochote katika yale mliyowapa wanawake, isipokuwa pale wote wawili watapochelea kuwa hawatoweza kusimamisha mipaka ya Allaah. Mtapochelea kuwa wote wawili hawatoweza kusimamisha mipaka ya Allaah, basi hakuna neno juu yao katika ambacho amejikombolea kwacho.”[1]

Kwa hiyo kutengana namna hii kunazingatiwa ni kujikomboa na fidia. Kisha Allaah (´Azza wa Jall) akasema:

فَإِن طَلَّقَهَا فَلَا تَحِلُّ لَهُ مِن بَعْدُ حَتَّىٰ تَنكِحَ زَوْجًا غَيْرَهُ

“Akimtaliki, basi hatokuwa halali kwake baada ya hapo mpaka aolewe na mume mwengine.”[2]

Ingelikuwa tunazingatiwa Khul´ ni talaka basi maneno Yake:

فَإِنْ طَلَّقَهَا

“Akimtaliki… “

ingelikuwa ni talaka ya nne, jambo ambalo linakwenda kinyume na maafikiano. Maneno Yake:

فَإِنْ طَلَّقَهَا

“Akimtaliki… “

bi maana talaka ya tatu.

فَلَا تَحِلُّ لَهُ مِن بَعْدُ حَتَّىٰ تَنكِحَ زَوْجًا غَيْرَهُ

“… basi hatokuwa halali kwake baada ya hapo mpaka aolewe na mume mwengine.”[3]

Dalili katika Aayah iko wazi. Kwa ajili hiyo Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameonelea kwamba kila mtengano ambao ndani yake kuna mwanamke kujikomboa au kutoa fidia basi ni Khul´ na sio talaka. Haijalishi kitu hata kama itatokea kwa tamko la aina ya talaka.  Haya ndio maoni yenye nguvu.

[1] 02:229

[2] 02:230

[3] 02:230

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ash-Sharh al-Mumti´ (12/467-470)
  • Imechapishwa: 05/05/2020