Makusudio ya kutengana katika biashara

Swali: Makusudio ya kutengana wakati wa biashara kunakuwa kwa miili au kwa kitu gani?

Jibu: Muulizaji anaashiria maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Watapouziana watu wawili basi kila mmoja katika wao ana khiyari midhali hawajatengana.”

Makusudio ya kutengana ni miili au maneno? Tunasema kuwa dhahiri ni kutengana kwa miili na kwamba unapomuuzia ndugu yako kitu, basi bado uko na khiyari maadamu bado mko katika kikao hata kama kitarefuka. Kwa mfano kama mtakuwa ndani ya gari na yeye ameketi kwenye siti nyingine ambapo akakuuzia kitu, midhali bado hamjafarikiana basi kila mmoja katika nyinyi yuko na khiyari. Lakini wote wawili wana haki ya kukata hiyo khiyari. Kwa mfano muuzaji anaweza kumwambia ´nakuuzia kwa sharti kwamba huna khiyari`. Mnunuzi akikubali basi hana khiyari. Haijalishi kitu hata kama atakuwa katika kikao hichohicho. Kwa ajili hiyo imekuja katika Hadiyht hiyohiyo:

“… midhali hawajatengana na wakawa pamoja au mmoja akamukhiyarisha mwingine.”

Mmoja akimwondoshea khiyari mwingine na wakakubaliana hilo, basi biashara imewajibika. Wakitengana kabla ya biashara kuvunjika, basi biashara imewajibika.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (57) http://binothaimeen.net/content/1295
  • Imechapishwa: 16/10/2019