Makatazo juu ya Tarawiyh za express

Swali: Imamu wetu wa msikiti anaharakisha sana katika swalah ya Tarawiyh. Hivyo tunashindwa kuomba du´aa, kusabihi wala kuwa na unyenyekevu katika fursa hii kubwa. Pamoja na hivyo hasomi isipokuwa ile Tashahhud ya kwanza tu “ash-Had an laa ilaaha illa Allaah wa ash-Had anna Muhammad Tasuulullaah” na anasema kwamba kusema hivi inatosha. Kwa msemo mwingine ni kwamba hamsalii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na anasema kwamba hiyo ni nyongeza. Kuhusu Aayah hasomi isipokuwa Aayah moja au mbili. Tunaomba nasaha na maelekezo.

Jibu: Kilichowekwa katika Shari´ah kwa maimamu katika Tarawiyh na katika swalah za faradhi ni kuwa na utulivu, kusoma kwa utulivu, kuwa na unyenyekevu katika Rukuu´, Sujuud, wakati wa kuinuka kutoka katika Rukuu´, kati ya sijda mbili na katika swalah nzima. Ni mamoja swalah hiyo ni ya faradhi au ni ya sunnah. Kuwa na utulivu ni jambo la lazima. Mwenye kuliharibu hilo basi swalah yake inabatilika. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Alimuona mtu anaswali na si mwenye utulivu katika swalah yake ambapo akamwamrisha kuirudi swalah yake na kuwa na akamwelekeza juu ya uwajibu wa kuwa na utulivu katika Rukuu´, Sujuud na kusimama kwa kunyooka baada ya kutoka Rukuu´ na kati ya sijda mbili.”[1]

Kilichowekwa katika Shari´ah kwa maimamu vilevile wasome kwa utulivu na wafanye unyenyekevu ndani yake ili yeye na wale waswaliji walio nyuma yake waweze kufaidika kwa kisomo chake. Jengine ni ili kwa kisomo hicho nyoyo ziweze kutikisika na kumuogopa Mola wake.

Jengine ni kwamba ni wajibu kwa imamu na kwa maamuma wamswalie Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) du´aa Ibraahimiyyah baada ya shahaadah mbili na kabla ya kutoa Tasliym. Kwa sababu imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba ameamrisha hilo. Kuna kundi la wanachuoni ambao wanaonelea kuwa hilo ni faradhi. Kwa hiyo haijuzu maimamu na kwa maamuma kupingana na Shari´ah takasifu katika swalah na katika mambo mengine.

Vilevile imewekwa katika Shari´ah kwa imamu, maamuma au ambaye anaswali peke yake kumuomba Allaah kinga dhidi ya Moto, adhabu ya kaburi, fitina ya uhai na ya kifo na fitina ya al-Masiyh ad-Dajjaal baada ya kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kabla ya kutoa Tasliym. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akifanya hivo na aliwaamrisha Ummah wake kusoma du´aa hiyo. Imependekezwa vilevile kuzidisha du´aa zengine kabla ya kutoa salamu. Mfano wa du´aa hizo ni ile du´aa inayotambulika ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimfunza Mu´aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ´anh) aiombe mwishoni au baada ya kila swalah:

اللهم أعني على ذكرك وشكرك وحسن عبادتك

“Ee Allaah! Nisaidie juu ya kuweza kukutaja, kukushukuru na kukufanyia uzuri ´ibaadah Yako.”

[1] al-Bukhaariy (6667), Muslim (397), at-Tirmidhiy (303), Abu Daawuud (856) na Ibn Maajah (1060).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (30/36-37)
  • Imechapishwa: 03/06/2018