Makafiri wa Quraysh ni wajuzi zaidi kuliko watu hawa

Swali: Mwenye kupeleka maana ya “Laa ilaaha illa Allaah” katika Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah na al-Haakimiyyah anazingatiwa ni miongoni mwa wale ambao makafiri wa ki-Quraysh ni wenye ufahamu zaidi yake?

Jibu: Bila ya shaka yoyote. Makafiri wa ki-Quraysh waliifahamu kwa njia ya Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Yeye ameifahamu kwa njia ya Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah.

Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah ni kitu kipo. Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah ipo kwa watu na hakuna walioipinga isipokuwa watu wenye kudhihirisha kuwa wanapinga. Vinginevyo ndani ya nafsi zao wanajua kuwa hakuna muumba, mruzukaji na mwenye kuyaendesha mambo isipokuwa Allaah. Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah ni kitu cha kimaumbile. Hakuna yeyote mwenye kuikanusha. Ingelikuwa inatosheleza basi kusingelikuwa na haja ya kutumilizwa Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Kila Mtume alikuwa akiwaambia watu wake:

لَقَدْ أَرْسَلْنَا نُوحًا إِلَىٰ قَوْمِهِ فَقَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ

“Kwa hakika Tulimpeleka Nuuh kwa watu wake akasema: “Enyi watu wangu! Mwabuduni Allaah.” (07:59)

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ

“Na Hatukutuma kabla yako Mtume yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: “Hakika hakuna mungu wa haki ila Mimi, basi niabuduni.”” (21:25)

Hakusema wakubali uola kwa sababu hiki ni kitu kilichopo. Jengine ni kwa sababu haitoshelezi.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Qaa´idah Jaliylah fiyt-Tawassul wal-Wasiylah (21) http://www.alfawzan.af.org.sa/node/2137
  • Imechapishwa: 09/07/2020