Swali: Unasemaje kuhusu vijana kama hawa wenye kupenda kuigiliza desturi zisizokuwa zetu wala hazitokamani na sisi kama mfano wa kufuga nywele mpaka kusipokuwa na mwisho, kurefusha nguo chini ya fundo mbili za miguu na kuweka cheni shingoni mwao? Je, matendo haya si ni haramu? Je, swalah na swawm za vijana hawa zinakubaliwa?

Jibu: Inafaa kuigiliza mambo yanayonufaisha ambayo Shari´ah haijakuja kuyakataza. Kuhusu kuigiliza katika mambo yanayodhuru au ada ambazo Shari´ah imekuja kuyakataza ni kitu kisichojuzu. Watu hawa ambao wanarefusha nywele zao mpaka kusipokuwa na mwisho ni jambo ambalo linakwenda kinyume na desturi inayofuatwa hii leo. Kufuga nywele za kichwani ni jambo wanachuoni wametofautiana kama ni Sunnah inayotakiwa kufuatwa au ni katika desturi ambazo mtu anatakiwa kutazama yale ambayo watu wamezowea katika zama zake. Maoni ninayoyapa nguvu ni kwamba kitendo hichi ni katika desturi ambazo mtu anatakiwa kufuata yale waliyozowea watu katika wakati wake. Ikiwa miongoni mwa desturi za watu ni kufuga nywele basi na yeye pia afanye. Na ikiwa desturi za watu ni kunyoa au kupunguza nywele basi na yeye pia afanye hivo.

Lakini balaa kubwa ni kwamba hawa watu ambao wanafuga nywele za vichwani mwao hawafugi ndevu zao. Kisha wanadai eti wanamuiga Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), jambo ambalo si la kweli. Ukweli wa mambo ni kwamba wanafuata matamanio yao. Dalili inanyoonyesha kuwa si wa kweli katika kumfuata kwao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kwamba utawaona wamepoteza kitu katika dini yao ambacho ni miongoni mwa mambo ya wajibu; kama mfano wa kufuga ndevu. Hawazifugi ndevu zao ilihali wameamrishwa kuzifuga. Jengine ni kwamba wanapuuzilia mbali swalah na mambo mengine ya wajibu. Haya yanakufahamisha kuwa matendo yao ya kufuga nywele za vichwani mwao malengo sio kumwabudu Allaah wala kumfuata Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hiyo ni desturi waliyoipenda tu na ndio maana wakaifanya.

Kuhusu kuvaa cheni ni jambo la haramu kwa sababu ni mambo ya wanawake. Huko ni kujifananisha na wanawake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemlaani mwanaume anayejifananisha na wanawake. Uharamu na dhambi inakuwa kubwa zaidi cheni hiyo ikiwa ya dhahabu. Jambo hilo ni haramu kwa mwanamke kwa njia mbili zote; kwa njia ya kwamba ni dhahabu na kwa njia ya kwamba anajifananisha na mwanamke. Ubaya unakuwa mkubwa zaidi ikiwa vazi hilo lina picha ya mnyama, mfalme, mkuu fulani au baya zaidi kuliko hayo ikiwa ni vazi la msalaba, kitendo ambacho ni haramu hata kwa mwanamke akivaa vazi hilo lina msalaba. Ni mamoja picha hiyo ni ya mtu, mnyama ya ndege au mnyama mwingine au vazi lenye picha ya msalaba. Kivazi kilicho na picha ni haramu kwa wanaume na kwa wanawake. Haijuzu kwa wote wawili kuvaa vazi lililo la picha ya mnyama au picha ya msalaba.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb (16) http://binothaimeen.net/content/6810
  • Imechapishwa: 18/03/2021