Madhehebu yetu ni madhehebu ya Salaf

Madhehebu yetu ni madhehebu ya Salaf. Tunathibitisha sifa pasi na kushabihisha na tunamtakasa Allaah pasi na kukanusha. Haya ndo madhehebu ya maimamu wa Uislamu kama mfano wa Maalik, ash-Shaafi´iy, ath-Thawriy, al-Awzaa´iy, Ibn-ul-Mubaarak, Imaam Ahmad na Ishaaq bin Raahuuyah. Madhehebu haya ndio yaliyofutwa na Mashaykh kama mfano wa Fudhwayl bin ´Iyaadhw, Abu Sulaymaan ad-Daaraaniy, Sahl bin ´Abdillaah at-Twustariy na wengineo. Hakuna yeyote katika maimamu hawa ambaye anaonelea kinyume katika misingi ya dini. Kadhalika Abu Haniyfah. ´Aqiydah iliyothibiti kwake ni yenye kuafikiana na ´Aqiydah ya watu hawa, nayo ni yale yaliyotajwa katika Qur-aan na Sunnah. Imaam Ahmad amesema:

“Allaah hasifiwi isipokuwa kwa yale aliyojisifia Mwenyewe au yale aliyomsifia kwayo Mtume Wake. Hatuvuki Qur-aan na Hadiyth.”

Haya pia ndio madhehebu ya wengineo. Hivyo tunawafuata Salaf katika jambo hili. Kwani wao ndio maimamu wajuzi zaidi inapokuja katika suala la kukanusha na kuthibitisha. Wao wanamuadhimisha Allaah na kumtakasa Allaah zaidi kutokamana na yale mambo yasiyostahiki Kwake. Hakika maana ya wazi yenye kufahamika katika Qur-aan na Sunnah hairudishwi nyuma kwa utata. Kuirudisha ni njia moja ya kukengeusha maandiko kutoka mahala pake stahiki. Wala haitakiwi kusema kwamba ni maandiko yasiyofahamika maana yake na wala hayafahamiki makusudio yake. Hili lingekumbushia wale wanaosoma Kitabu pasi na kukifahamu. Uhakika wa mambo ni kwamba ni Aayah zilizo waziwazi. Zinafahamisha maana tukufu na ya wazi iliyosimama kwenye nyoyo za wanachuoni.

  • Mhusika: Imaam Swiddiyq Hasan Khaan al-Qanuujiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qatf-uth-Thamar, uk. 57-58
  • Imechapishwa: 29/01/2019