Mada hii inahitajia busara


Swali: Kuna suala linaloandikwa sana na chini ya jina la “Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah” ilihali ukweli wa mambo ni mfumo wa Khawaarij. Kwa hivyo tulikuwa tunapendelea kuthibitisha suala hili. Suala lenyewe linahusiana na utungaji wa sheria unaohukumiwa na watawala. Wanajengea hoja kwa fatwa yako katika “al-Majmuu´ ath-Thamiyn” na kwamba hiyo ni kufuru ya wazi kwa sababu inahusiana na ubadilishaji. Maoni hayohayo yananasibishwa kwa Shaykh Muhammad bin Ibraahiym [Aalus-Shaykh] (Rahimahu Allaah). Ili swali liwe la wazi ni kama ifuatavyo; kinachozingatiwa ni vile vikwazo vya Takfiyr au ni ile Iqaamat-ul-Hujjah ilioshurutishwa na Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kwa yule mwenye kuhukumu uwekaji wa sheria wa jumla kinyume na yale aliyoteremsha Allaah?

Jibu: Ni lazima kwa kila mtu mwenye kutenda kitendo cha ukafiri kusiwepo vizuizi vya ukafiri. Kwa ajili hii imetajwa katika Hadiyth Swahiyh wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoulizwa kama inafaa kwao kuwapiga vita watawala ambapo akasema:

“Mpaka pale mtakapoona ukafiri wa wazi ambao mna dalili kwayo kutoka kwa Allaah.”

Ni lazima kufuru iwe ya wazi inayotambulika ambayo haina sintofahamu. Ikiwa iko na sintofahamu, basi hakufurishwi mwenye nayo ijapo tutasema kuwa kitendo chenyewe ni ukafiri. Kwa hivyo inatakiwa kupambanua kati ya maneno na msemaji na kitendo na mtendaji. Kitendo kinaweza kuwa dhambi nzito pasi na mtendaji kuwa mtenda dhambi nzito kwa sababu ya kuwepo vikwazo vinavyomzuia kumtia katika ufuska. Kinaweza vilevile kikawa ni ukafiri pasi na mtendaji mwenyewe kuwa kafiri kwa sababu ya kuwepo vikwazo vinavyomzuia kumtia katika ukafiri.

Hakuna chochote zaidi ya sintofahamu hii mbaya iliyofanya uasi wa Khawaarij kuudhuru Ummah wa Kiislamu. Khawaarij wanafahamu kimakosa kwamba kitendo ni ukafiri na hivyo wanafanya uasi, kama walivyomwambia ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh). Walikuwa pamoja na ´Aliy bin Abiy Twaalib katika jeshi la Shaam. Wakati kulipotokea suluhu kati ya ´Aliy bin Abiy Twaalib na watu wa Shaam, ndipo Khawaarij wakamfanyia uasi baada ya kwamba walikuwa pamoja naye. Akawapiga vita na kuwaua na himdi zote njema anastahiki Allaah. Nukta muhimu ni kwamba walimfanyia uasi na wakasema:

“Umehukumu kinyume na yale aliyoteremsha Allaah. Umewafanya watu kuhukumu.”

Matokeo yake wakajivua kutoka katika utiifu wake. Janga la Ummah linatokana na tafsiri za kimakosa. Mtu anaweza kufikiria kimakosa kwamba kitu fulani ni ukafiri wa wazi na hivyo akafanya uasi. Kuna uwezekano pia kitendo fulani kweli ni ukafiri lakini mtendaji akawa sio kafiri kwa sababu ya kuwepo vikwazo. Mfanya uasi huyu akaonelea kuwa mtu huyo hana udhuru na hivyo akafanya uasi.

Kwa ajili hiyo mtu anatakiwa kutokuwa na haraka ya kuwakufurisha watu au kuwatia katika ufuska. Pengine mtu akafanya dhambi nzito ya wazi, lakini pasi na kujua. Anapofikishiwa kuwa ni haramu, akashukuru na kuachana nayo. Je, haya hayapatikani? Hapana shaka yanapatikana. Vipi basi nitamhukumu mtu kuwa ni mtenda dhambi nzito bila ya kumsimamishia hoja?

Hawa ambao umewaashiria kati ya watawala wa kiarabu na waislamu pengine wakawa ni wenye kupewa udhuru. Pengine hawajafikishiwa haki. Pengine vilevile wamefikishiwa haki lakini baadaye kwa mfano akaja mtu kuwafanya kuwa na sintofahamu katika masuala. Kwa hivyo ni lazima kwa mtu kuwa makini katika suala hili.

Hebu wacha tuseme kuwa sharti zimekamilika za kufaa kumfanyia uasi kwa njia ya kwamba tumeona ukafiri wa wazi ambao tuna dalili kwao kutoka kwa Allaah. Ni sharti ionekane kufuru hiyo. Ukafiri ni sharti. Kuwa kwake ya wazi ni sharti. Iwe na dalili kutoka kwa Allaah ni sharti. Ni sharti nne. Maneno yake “Mpaka pale mtakapoona… “ ili mtu asije kutumbukia katika tetesi zisizokuwa na uhakika wowote. Hiyo ina maana kwamba mtu ajue elimu ya yakini. Maneno yake “ukafiri” ili mtu asije kuchanganya na dhambi nzito. Ikiwa mtawala ni muovu anayekunywa pombe bila ya kuingia ndani ya ukafiri, basi haitofaa kumfanyia uasi. Maneno yake “ya wazi” bi maana ya wazi kabisa isiyokuwa na sintofahamu. Maneno yake “ambao mna dalili kwayo kutoka kwa Allaah”. Hiyo inaa maana kwamba isiwe ya wazi kwa mujibu wa mtazamo wetu. Bali sisi tutegemee dalili ya wazi na ya kukata kabisa. Hizi ndio sharti nne za kufaa kufanya uasi.

Hata hivyo ipo sharti ya tano ili kufanya uasi kuwe ni lazima. Ikifaa kwetu kufanya uasi kwa mtawala ni lazima kwetu kufanya uasi huo? Mtu anatakiwa kutazama manufaa. Je, sisi tunao uwezo wa kumng´oa? Hivyo basi tutafanya hivo. Ikiwa hatuna uwezo wa kufanya hivo, hatutofanya uasi. Mambo yote ya wajibu ya Shari´ah yanatumika kunapokuwa na uwezo wa kuyatekeleza.

Na pengine kama tuna uwezo wa kufanya uasi, pengine uasi huo ukapelekea katika madhara makubwa na mazito zaidi kuliko mtu huyu kuendelea kubaki kama kiongozi. Tukimfanyia uasi na yeye akashinda, basi tutadhalilishwa zaidi na wakati huohuo yeye azidi katika kuchupa kwake mipaka na ukafiri wake.

Masuala haya yanahitajia akili iliokomaa na akili hiyo iambatanishwe na Shari´ah na yasihukumiwe na hisia. Sisi tunahitajia hisia kwa sababu ya kuwa na hamasa na tunahitajia Shari´ah ili ituambatanishe. Ni lazima tuwe na breki. Gari pasi na breki inagonga na gari pasi na umeme haiendeshwi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa' al-Baab al-Maftuuh (51 B)
  • Imechapishwa: 16/08/2021